HIZI HAPA REKODI NA TAKWIMU ZA LIGI KUU YA NBC 2022/2023.

DURU la 22 Ligi Kuu ya NBC ikielekea kuanza februari 3, Kwa mchezo kati ya Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar uwanja wa Sokoine, Mbeya na Simba ikiikaribisha Singida Big Stars uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam rekodi mbalimbali zimewekwa na baadhi ya wachezaji mpaka kufikia duru la 21.

Zifuatazo ni rekodi na takwimu za kipekee zilizowekwa na wachezaji na timu za Ligi Kuu ya NBC mpaka kufikia duru la 21;

John Bocco wa timu ya Simba ndiye kinara wa kufunga mabao matatu (Hat-Trick) katika mechi akiwa amefanya hivyo katika michezo miwili dhidi ya timu za Tanzania prisons na Ruvu Shooting huku wachezaji wengine waliofunga idadi hiyo ya mabao kwenye mchezo mmoja wakiwa Fiston Mayele (Yanga) dhidi ya Singida BS, Saido Ntibanzokiza (Simba) dhidi ya Prisons na Ibrahim Mkoko (Namungo) aliyefunga dhidi ya KMC .

Nickson Kibabage ndiye mchezaji aliyefunga bao la mapema Zaidi mpaka raundi ya 21, akifanya hivyo katika mchezo kati ya Mtibwa Sugar na Mbeya City Kwenye uwanja wa Manungu, Morogoro.

Timu ya Dodoma Jiji inaongoza kwa kupata mikwaju mingi ya penati (sita) huku ikiongoza pia katika kukosa penati hizo ikikosa tano na kufanikiwa kufunga penati moja pekee huku Mbwana Kibacha wa timu hiyo akiongoza kwa kukosa penati nyingi (2).

Sebusebu Samson mchezaji wa Geita Gold ni golikipa pekee aliyepiga pasi iliyozaa bao mpaka sasa akifanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya Polisi Tanzania katika uwanja wa Nyankumbu, Geita bao lililofungwa na Elias Maguli.

Timu ya Simba mpaka sasa ni timu pekee iliyofunga idadi kubwa ya mabao katika mchezo mmoja dhidi ya Tanzania Prisons kwa ushindi wa mabao 7-1 mchezo uliochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mayele wa timu ya Yanga ameendelea kushikilia usukani katika vinara wa ufungaji akiwa na mabao 15 akimzidi Moses Phiri wa timu ya Simba mwenye mabao 10 anayeshika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao matano.

Ntibazonkiza wa Simba amehusika katika mabao 17 (mabao tisa na pasi nane za mabao) akifuatiwa na Mayele wa Yanga aliyehusika katika mabao 17 (mabao 15 na pasi za mabao mbili) na Clatous Chama wa Simba akishika nafasi ya tatu akihusika katika mabao 15 (mabao matatu na pasi 12 za mabao).

Mchezaji wa Simba Clatous Chama ameendelea kushika nafasi ya kwanza kwenye vinara wa kutoa pasi za mabao (12) huku nafasi ya pili ikishikwa na Saido Ntibazonkiza akiwa na pasi nane za mabao na Ayoub Lyanga wa Azam akikamata nafasi ya tatu na pasi saba za mabao.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *