Author: Yahaya Abushehe

MTIBWA

MTIBWA YAISHUSHIA MVUA YA MABAO GEITA, NBC CHAMPIONSHIP IKIENDELEA.

JUMLA ya mabao 13 yamefungwa  kwenye michezo mitano (5) ya Ligi ya Championship ya NBC iliyochezwa leo Februari 26, 2025 kwenye mikoa minne tofauti.

Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani kwake Manungu mkoani Morogoro imeibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Geita Gold mpinzani wake wa karibu kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC, kwa matokeo hayo Mtibwa inasalia kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikifikisha alama 51 kwenye michezo 21 iliyocheza.

Transit Camp ikiwa nyumbani ikakubali kichapo cha bao 0-1 dhidi ya Green Warriors, Cosmopolitan ikapokea kichapo cha bao 0-1 dhidi ya Kiluvya huku Bigman ikiifunga Biashara UTD kwa bao 2-0.

Mchezo wa Mwisho kwa leo ulizikutanisha Mbuni dhidi ya Mbeya City ambapo Mbeya City ikiwa ugenini ikaibuka na ushindi wa mabao 1-3, ushindi huu unaipandisha Mbeya City hadi nafasi ya tatu (3) kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho Februari 27 kwa michezo miwili (2) kuchezwa ambapo African Sports itakuwa mwenyeji wa Polisi Tanzania huku TMA ikiwakaribisha Songea United.

MTIBWA VS GEITA

MTIBWA, GEITA VITA YA UONGOZI NBC CHAMPIONSHIP.

JUMLA ya mechi tano (5) zinachezwa leo Februari 26, 2025 kwenye mikoa ya Lindi, Pwani, Morogoro na Arusha huku michezo yote ikianza saa 10:00 alasiri.

Mchezo unaosubiriwa kwa hamu hii leo unazikutanisha Mtibwa Sugar dhidi ya Geita Gold kwenye uwanja wa Manungu mkoani Morogoro, Mtibwa inaongoza msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 48 huku Geita Gold ikishika nafasi ya pili ikiwa na alama 45.

Upekee wa mchezo huu ni kuwa yeyote anayeshinda anakaa kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC, Mchezo wa Duru ya kwanza uliochezwa kwenye uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita, Geita Gold ilishinda kwa bao 1.

Mkoani Lindi Bigman FC itaialika Biashara United, Cosmopolitan itakuwa mwenyeji wa Kiluvya Jamhuri – Morogoro, kwenye uwanja wa Mabatini mkoani Pwani Transit Camp itawapokea Green warriors, mchezo wa mwisho kwa leo utazikutanisha Mbuni dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

SIMBA VS AZAM

MZIZIMA ‘DERBY’ HAKUNA MBABE.

HAKUNA Mbabe ndivyo unavyoweza kusema baada ya mchezo wa ‘Derby’ ya mzizima kati ya Simba SC na Azam FC kutamatika kwa sare ya mabao 2-2 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mabao ya Azam FC yamefungwa na Gibrill  Sillah na Zidane Sereri huku yale ya Simba SC yakifungwa na Elie Mpanzu na Abdulrazack Hamza.

Zidane Sereri wa Azam FC alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo, Zidane aliyecheza dakika 10 pekee alihusika kwenye bao la mwisho la Azam FC ambalo liliihakikishia Azam FC kupata alama moja kwenye mchezo huo.

Simba inendelea kusalia nafasi ya pili ikiwa na alama 51 baada ya michezo 20 wakati Azam FC ikiwa nafasi ya tatu ikiwa na alama 44 kwenye michezo 21 ya Ligi Kuu ya NBC.

MZIZIMA DERBY

NANI KUIBUKA MBABE WA MZIZIMA ‘DERBY’ LEO ?

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Februari 24, 2025 kwa mchezo mmoja wa ‘Derby’ ya Mzizima kati ya Simba SC na Azam FC kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia majira ya saa 1:00 usiku.

Simba inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na alama 50 baada ya michezo yake 19 huku ikifunga mabao 41 na kuruhusu sita (6) pekee.

Kwa upande wa Azam FC ina jumla ya alama 43 baada ya michezo 20 ya Ligi Kuu ya NBC ikifunga mabao 29 na kuruhusu tisa (9) pekee.

Mara ya mwisho timu hizi zilikutana Septemba 26, 2024 visiwani Zanzibar, na mchezo huo kumalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Kila timu imefanya maboresho kwenye kikosi chake katika dirisha dogo la usajili ambapo Simba imemuongeza kikosini Elie Mpanzu huku Azam FC ikiwasajili Zidane Sereri na Landry Zouzou.

LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC KINAPIGWA SANA

LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC ‘KINAPIGWA’ SANA

TAYARI mizunguko 19 ya Ligi ya Championship ya NBC imeshachezwa hadi sasa na kushuhudiwa kwa ushindani mkubwa wa nafasi kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Mtibwa Sugar inaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi hiyo ikiwa na alama 45 ikifuatiwa na Geita Gold kwenye nafasi ya pili ikiwa na alama 42, Stand United ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 39 huku nafasi ya nne ikishikiliwa na Mbeya City ikiwa na alama 39.

Biashara United inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama nne pekee hadi sasa, Cosmopolitan inashikilia nafasi ya 15 moja kutoka mwisho ikiwa na alama tisa.

Timu mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC zinapanda moja kwa moja Ligi Kuu ya NBC huku zile mbili za mwisho zikishuka moja kwa moja hadi First League.