Author: Yahaya Abushehe

Yanga yarejea kileleni ligi kuu ya nbc

YANGA YAREJEA KILELENI, KAGERA GARI LIMEWAKA.

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana Februari 14, 2025 kwa michezo minne kupigwa kwenye mikoa ya Tabora, Dar es Saalam, Mbeya na Kagera.

Mchezo wa mapema saa 8:00 Mchana ulizikutanisha Tabora United dhidi ya Kengold na kumalizika kwa sare ya bao moja, Bao kwa upande wa Kengold likifungwa na Selemani Bwenzi kwa mkwaju wa penati na kufikisha mabao matatu kwenye michezo mitatu ya Ligi Kuu ya NBC aliyocheza mpaka sasa huku bao la Tabora United la kusawazisha likifungwa na Heritier Makambo na kufikisha jumla ya mabao sita kwenye Ligi Kuu ya NBC mpaka sasa.

Mkoani Mbeya, Tanzania Prisons ikaialika Namungo kwenye uwanja wa  Sokoine saa 10:00 alasiri na kumalizika kwa Namungo kuibuka na ushindi wa bao moja, ushindi huo unaipandisha Namungo hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikifikisha Alama 21.

Young Africans ikiwa ugenini KMC Complex, Dar es Salaam ikaibuka na ushindi mnono wa mabao 1-6 dhidi ya KMC na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikifikisha alama 49 kwenye michezo 19 ya Ligi Kuu ya NBC, Young Africans imefunga jumla ya mabao 48 mengi zaidi kuliko timu yoyote kwenye Ligi Kuu ya NBC mpaka sasa.

Kagera Sugar ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani Kaitaba mkoani Kagera, imepata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, imewachukua takribani siku 102 kwa Kagera Sugar kupata ushindi kwenye uwanja wake wa nyumbani kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu, Mara ya mwisho Kagera kupata ushindi ilikuwa ni Novemba 4, 2024 dhidi ya Dodoma Jiji ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Ligi hiyo inaendele leo Februari 15, 2025 kwa michezo miwili, mchezo wa kwanza ukizikutanisha Pamba Jiji dhidi ya Coastal Union saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza huku Mchezo wa pili na wa mwisho ukizikutanisha Azam FC dhidi ya Mashujaa kwenye uwanja wa Azam Complex saa 1:00 usiku.

SINGIDA YABEBA ALAMA TATU LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea leo Februari 13, 2025 kwa mchezo mmoja kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ukizikutanisha JKT Tanzania dhidi ya Singida Black Stars na kumalizika kwa Singida kushinda kwa bao 1.

Bao pekee la Singida Black Stars hii leo limefungwa na Jonathan Sowah dakika ya 52 ya mchezo akimalizia kazı iliyofanywa na Arthur Bada.

Kwa ushindi huo Singida Black Stars inaendelea kusalia nafasi ya 4 kwenye msimamo ikifikisha alama 37 baada ya michezo 19.

Katika hatua nyengine mchezaji Jonathan Sowah amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na mchango wake mkubwa kwa timu yake kuondoka na alama tatu akifunga bao pekee na la ushindi kwa Black Stars.

LIGI KUU YA NBC

LIGI KUU YA NBC KUCHEZWA ARUSHA, SINGIDA LEO.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Februari 7, 2025 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Arusha na Singida kuanzia saa 10:00 Alasiri.

Mkoani Arusha Coastal Union itaikaribisha JKT Tanzania kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid huku ikiingia kwenye mchezo huu ikishika nafasi ya 11 ikikusanya alama 18 kwenye michezo 16 na JKT Tanzania ikishika nafasi ya nane baada ya kukusanya alama 19 wakiwa na tofauti ya alama moja (1) pekee kati yao.

Mkoani Singida, timu ya Singida Black Stars itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar ya mkoani Kagera kwenye uwanja wa CCM Liti huku mara ya mwisho timu hizi kukutana Agosti 24, 2024 mkoani Kagera, Singida Black Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 likifungwa na Mchezaji Anthony Tra Bi dakika ya 90+3 ya mchezo huo.

Michezo hii miwili inakamilisha michezo ya mzunguko wa 17 wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 ambapo mpaka sasa timu ya Young Africans ikishika usukani na alama 45 huku Kengold ikiburuza mkia ikiwa na alama sita pekee.

 

MTIBWA WABABE WA NAMBA NBC CHAMPIONSHIP MPAKA SASA.

JUMLA ya Michezo 136 kati ya 240 imeshachezwa kwenye Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/2025 na kushuhudia jumla ya mabao 297 yakifungwa kwenye michezo hiyo huku Mtibwa Sugar ikiwa kinara kwa kufunga mabao mengi.

Mtibwa imefunga jumla ya mabao 31 kwenye michezo 17 mengi zaidi kuliko timu yeyote kwenye Ligi ya Championship ya NBC hadi sasa huku ikiruhusu kufungwa mabao saba pekee machache zaidi kuliko timu yeyote kwenye Ligi hiyo.

Mtibwa inaongoza msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 44 baada ya michezo 17 ikishinda michezo 14 ikipata sare michezo miwili na kufungwa mchezo mmoja pekee.

 

MZUNGUKO WA 17 NBC CHAMPIONSHIP KUKAMILIKA LEO.

MZUNGUKO wa 17 wa Ligi ya Championship ya NBC unatamatika leo kwa mchezo kati ya Transit Camp ya Dar es salaam na Stand United ya Shinyanga saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Mabatini Mkoani Pwani.

Transit Camp ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 10 sawa na Kiluvya iliyo nafasi ya 14 zikitofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa huku Stand United ikiwa nafasi ya nne (4) na alama 32.

Mpaka sasa Mtibwa Sugar inaongoza kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 44 kwenye michezo 17 wakati Biashara United ikishika nafasi ya mwisho ikiwa na alama nne (4) pekee kwenye michezo 17