Category: STORY

MBEYA CITY YAFUTA ‘UTEJA’ KWA NAMUNGO

Timu ya Mbeya City imemaliza uteja wake wa kupoteza mechi dhidi ya Namungo kwa kuifunga mabao 2-1 na kupanda nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu NBC

Mchezo huo wa tano kwa Mbeya city wakicheza katika uwanja wa nyumbani ulishuhudia mabao ya timu hiyo yakifungwa na Sixtus Sabilo na Hassan Muhamud huku bao pekee la Namungo likifungwa na Reliants Lusajo akifikisha mabao sita na kuwa kinara wa wafungaji katika Ligi ya NBC

Matokeo hayo yanaifanya Mbeya City kufikisha alama 15 baada ya mechi tisa huku Namungo wakisalia na alama 15 baada ya kucheza mechi 10

Mchezo huo ulishuhudiwa ukimalizika Dakika zote 90 bila mchezaji yeyote kuonyeshwa kadi ya njano wala nyekundu

Ligi hiyo itaendelea tena Novemba 6 kwa mchezo kati ya Polisi Tanzania dhidi ya Singida Big Stars katika uwanja wa Black Rhino Academy uliopo Karatu mkoani Arusha .

NAMUNGO KUENDELEZA UBABE KWA MBEYA CITY LEO?

Timu ya Mbeya City leo inaikaribisha timu ya Namungo kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya katika muendelezo wa michezo ya Ligi Kuu ya NBC kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mbeya City inashuka uwanjani ikiwa na rekodi mbaya dhidi ya Namungo ikifanikiwa kushinda mechi moja kati ya sita zilizopita, ikipata sare moja na kupoteza mechi nne.

Namungo inaingia katika uwanja huo wa Sokoine ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kulazimishwa sare katika dakika za nyongeza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons baada ya mchezaji wake Frank Magingi kushindwa kuokoa mpira na kujifunga.

Mchezo huu wa leo ni wa ufunguzi wa raundi ya 11 itakayoshudia michezo mingine sita ikipigwa katika viwanja tofauti huku mchezo mmoja, Coastal Union dhidi ya Dodoma Jiji ukitarajiwa kupangiwa tarehe nyingine.

WARATIBU WA MICHEZO WAPIGWA MSASA

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kwa kushirikiana na TFF jana Septemba 22, 2022 iliandaa semina ya waratibu wa michezo iliyofanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es saalam.
Semina hiyo ilikuwa na lengo la kuwaongezea ufanisi waratibu hao katika kusimamia michezo mbalimbali ya kimashindano iliyochini ya TFF na TPLB.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Steven Mnguto, aliwataka waratibu kuzingatia mafunzo watakayopewa na wakufunzi kwani mafunzo hayo yanafaida kubwa kwenye ufanisi wa Ligi.
“Sisi Bodi ya Ligi peke yetu hatuwezi nyinyi mmekua msaada mkubwa sana kwetu, zingatieni mafunzo mnayopewa kwani mmepata bahati ya kufundishwa na watu waliokatika mpira kwa muda mrefu na wabobezi.” Alisema Steven Mnguto.
Semina ilihusisha mafunzo ya nadharia na vitendo ambapo waratibu wa michezo walipata nafasi ya kufanya yale waliyofundishwa darasani.
Wakati wa kufunga semina hiyo Mkurugenzi wa mashindano wa TFF Salum Madadi aliwapongeza waratibu kwa kazi nzuri wanayoifanya.
“Sponsors (wadhamini) wanajenga Imani kubwa na shirikisho kutokana na kazi kubwa mnayoifanya, mwisho kabisa niwatakie utekelezaji mwema wa msimu wa 2022/2023.” Alisema Salum Madadi.
Semina hiyo ilihudhuriwa na waratibu kutoka mikoa zaidi ya 22 Tanzania Bara na wengine kutoka Zanzibar Pamoja na watumishi wa Bodi ya Ligi na TFF.

SIMBA, PRISONS NI REKODI NA HISTORIA LEO MBEYA,YANGA YAPANDA KILELENI

Kivumbi cha raundi ya nne ya Ligi Kuu ya NBC kinaendelea leo kwa mchezo mmoja kati ya Tanzania Prisons na Simba utakaochezwa saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mchezo wa mwisho kwa timu hizi kukutana ilikuwa ni Juni 26, 2022 kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya na Tanzania Prisons kuibuka na ushindi wa bao moja lililofungwa na Benjamin Asukile.

Mara ya mwisho kwa Simba kupata matokeo katika uwanja ugenini dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa ni Mei 5, 2019 waliposhinda kwa bao moja.

Jana michezo miwili ya raundi ya nne ilichezwa, Mbeya City wakiwaalika Azam FC ulitamatika kwa Azam kushinda kwa bao moja, Saa 1:00 usiku Yanga SC waliwakabili Mtibwa Sugar na kumalizika kwa Yanga kushinda kwa mabao matatu, ushindi huo unawapandisha Yanga hadi nafasi ya kwanza ya msimamo.

RAUNDI YA NNE KUANZA LEO MBEYA ,YANGA MTIBWA VITANI

Ligi kuu ya NBC inaendelea hii leo kwa michezo miwili ya raundi ya nne, saa 10:00 alasiri Mbeya City watawaalika Azam FC kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Kwenye michezo mitano ya mwisho ya Ligi Kuu kwa timu hizi kukutana, Azam wameshinda mara tatu, Mbeya City wakishinda mchezo mmoja huku wakitoka sare mchezo mmoja.

Saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga SC watawakabili Mtibwa Sugar.

Kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Mtibwa Sugar wapo nafasi ya pili wakiwa na alama saba sawa na Yanga wenye alama saba, timu yoyote itakayopata ushindi kwenye mchezo wa leo itapanda moja kwa moja kwenye nafasi ya kwanza ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.