DODOMA, SINGIDA ZATOSHANA NGUVU LIGI KUU YA NBC.

UKIWA mchezo wa kwanza unaorejesha ladha za Ligi Kuu ya NBC baada ya kusimama kwa takribani wiki tano umeshuhudia timu za Dodoma Jiji na Singida Black stars zikimaliza kwa sare ya bao moja na kugawana alama kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua ulishuhudia mabao ya timu zote mbili yakipatikana dakika za ‘jioni’ kwa mikwaju ya penati iliyopigwa na Yasin Mgaza (Dodoma) dakika ya 83 na Marouf Tchakei (Singida) dakika ya 96.

Hii ni sare ya nne kwa timu ya Dodoma Jiji msimu huu huku ikuwa sare ya tatu kwa timu ya Singida Black Stars inayoiwakilisha Tanzania na Ligi ya nne kwa ubora Afrika (NBC) kwenye mashindano ya kimataifa msimu huu.

Akizungumza baada ya mchezo kocha mkuu wa Dodoma Jiji Amani Josiah amesema kukosa umakini kwa wachezaji wake kumesababisha kupoteza alama tatu na kuipata alama moja ingawa amewasifu kwa kiwango walichoonyesha ingawa mpinzani wao (Singida BS) alikuwa mgumu.

”Tumepata bao kipindi cha pili japo kipindi cha kwanza tumetengeneza nafasi nzuri za kupata mabao na endapo tungezitumia vizuri tungepata ushindi, yote kwa yote nawasifu wachezaji wangu wamepambana sana na hii alama moja tuliyoipata itatusaidia kutujenga huko mbele tunapoelekea” alisema Josiah.

Naye kocha mkuu wa Singida BS David Ouma raia wa Kenya amewasifu Dodoma kwa matumizi ya mipira mirefu iliyowapa changamoto wachezaji wake ingawa amewasifu vijana wake pia kwa kuonyesha mchezo mzuri.

”Mbinu waliyokuja nayo Dodoma kupiga mipira mirefu ilivuruga wachezaji wangu nyuma na kuwapa faida wao na endapo tungefanikiwa kuzuia mipira hiyo kipindi cha kwanza ingetusaidia kupata matokeo bora zaidi leo. Naamini kurejea kwa ligi kutatusaidia kuendelea kujijenga na kuwa bora zaidi katika michezo inayokuja” Alisema Ouma.

 

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *