LIGI ya Championship ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwa mzunguko wa 15 huku viwanja vya Ilulu, Lindi na TFF Center Kigamboni vikitarajiwa kutimua vumbi leo.
Bigman ya Lindi itakuwa mwenyeji wa Geita Gold inayoshika usukani wa Ligi ya Championship ya NBC kwenye uwanja wa Ilulu huku timu ya Bigman ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kulazimishwa sare kwenye uwanja huo na timu ya African Sports katika mchezo uliopita.
Hadi sasa timu ya Bigman imepoteza michezo mitano ya ligi hiyo na inakutana na Geita Gold ambayo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa huku ikitoka sare michezo mitatu pekee.
Kwenye uwanja wa TFF Center Kigamboni timu ya Transit Camp itakuwa mwenyeji wa ‘wababe’ kutoka mbeya timu ya Kengold iliyoshiriki Ligi Kuu ya NBC msimu uliopita.
Transit Camp iliyopoteza mchezo uliopita kwa kipigo kikali cha mabao 3-0 dhidi ya Mbuni ugenini itashuka uwanjani kupambana na Kengold iliyopoteza pia ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya B19 inayoshika nafasi ya 13 kwenye msimamo huku ikiifanya B19 kufikisha ushindi wa pili msimu huu.
Transit Camp inahitaji kushinda mchezo wa leo ili kuweka hai matumaini ya kupanda daraja na kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo hadi sasa nyuma ya vinara Geita Gold, Kagera Sugar na Mbeya Kwanza.