KYARUZI,SIMCHIMBA WANG’ARA TUZO ZA NBC CHAMPIONSHIP

BEKI wa Mtibwa Sugar  Erick Kyaruzi amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Januari wa Ligi ya NBC Championship 2024/25, huku Awadh Juma wa Mtibwa Sugar akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Kyaruzi aliyeingia fainali katika mchakato huo na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Boniface Maganga wa Mbeya Kwanza, alionesha kiwango chenye mwendelezo katika safu ya ulinzi, huku pia akisaidia timu yake kwa kufunga mabao mawili katika dakika 270 za michezo mitatu aliyotumika.

Kwa upande wa Awadh aliyeingia fainali na Zuberi Katwila wa Bigman na Emmanuel Massawe wa Mbeya Kwanza, aliiongoza timu yake kupata ushindi katika michezo yote mitatu iliyocheza ikivuna pointi tisa na kuendelea kuongoza ligi hiyo.

Pia kamati imemchagua Andrew Simchimba wa Geita Gold kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Februari wa Ligi ya NBC Championship 2024/25, huku Mohamed Muya pia wa Geita Gold akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Simchimba aliyeingia fainali katika mchakato huo na Oscar Tarimo wa Mbeya Kwanza na Mwisho Yangson wa Polisi Tanzania alionesha kiwango chenye mwendelezo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne katika michezo mitatu kwa dakika 253 alizocheza.

Kwa upande wa Muya aliyeingia fainali na Zuberi Katwila wa Bigman na Juma Hussein wa Stand United, aliiongoza timu yake kushinda michezo minne kati ya mitano iliyocheza mwezi huo.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *