Simba Kileleni

SIMBA YAPAA KILELENI, JKT, AZAM ZATOSHANA NGUVU LIGI KUU YA NBC

TIMU ya Simba imepaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuichapa timu ya Namungo mabao 3-0 kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Simba ilifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika mbili kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika kupitia kwa Karaboue Chamou kwa kichwa baada ya mpira wa kona uliopigwa na Joshua Mutale.

SIMBA VS NAMUNGO
SIMBA VS NAMUNGO

Dakika ya 61 Rushine De Reuck aliiandikia Simba bao la pili kwa pasi ya mpira uliokufa iliyopigwa na raia mwenzake wa Afrika Kusini Neo Maema.

Dakika ya 83 Mtanzania Selemani Mwalimu alifungua akaunti yake ya mabao kwenye Ligi Kuu ya NBC baada ya mabeki wa Namungo kushindwa kuokoa mpira kwenye eneo lao.

Kocha wa Namungo Juma Mgunda alisema timu yake ilizidiwa kimbinu na ukomavu hivyo watajifunza ili kujiimarisha na michezo ijayo.

” Tumejifunza, kuna wachezaji wadogo ambao wapo kwenye timu yangu wameona namna ya kucheza na timu kubwa hivyo hili ni funzo kwetu wakati mwingine tutafanya vizuri” Alisema Mgunda.

Rushine De Reuck mlinzi wa timu ya Simba alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo akifunga bao na kumaliza mchezo huo bila kuruhusu bao huku ikiwa mchezo wa pili mfululizo kwa Simba kucheza bila kuhurusu bao. 

JKT TANZANIA VS AZAM FC

Mchezo wa mapema uliopigwa saa 12:00 jioni uliozikutanisha timu za JKT Tanzania na Azam kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo mkoani Dar es Salaam na kushuhudia zikitoka sare ya bao moja.

Azam ilikuwa ya kwanza kuandika bao kupitia kwa kinara wa pasi za mabao msimu wa 2024/25 Feisal Salum dakika ya 42 lililosimama hadi mapumziko na kuwafanya ‘Maafande’ wa JKT Kwenda mapumziko vichwa chini.

JKT TANZANIA VS AZAM FC
JKT TANZANIA VS AZAM FC

Kipindi cha pili JKT ilirudi imara na dakika ya 90 Paul Peter aliisawazishia kwa mpira wa kichwa uliomshinda golikipa wa Azam Issa Fofana.

Paul Peter wa JKT Tanzania alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha ikiwa ni Pamoja na kuisaidia timu yake kupata bao la kusawazisha na kuendeleza rekodi ya mchezo wa tatu bila kupoteza.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *