Tag: #LIGIKUU #NBCPL #AZAM #YANGA #SIMBA #KMC #JKT #MASHUJAA #KENGOLD #DODOMAJIJI #PAMBAJIJI #KAGERASUGAR #SINGIDABLACKSTARS #FOUNTAINGATE #NAMUNGO

RATIBA YA LIGI KUU YA NBC MSIMU WA 2025/26 YAWEKWA WAZI.

KAIMU Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Ibrahim Mwayela ametangaza rasmi kuanza kwa Ligi Kuu ya NBC msimu 2025/2026 inayotarajiwa kufungua pazia Septemba 17 kwa michezo miwili itachezwa katika viwanja vya KMC, Dar es Salaam na Mkwakwani mkoani Tanga.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwayela amesema kuwa maandalizi yote kuelekea kuanza kwa msimu mpya yapo tayari kwa upande wa usimamizi wa ligi Kuu ya NBC Pamoja na vilabu.

“Ligi Kuu ya NBC inarejea rasmi Septemba 17 ambapo siku hiyo kutakuwa na michezo miwili KMC itaikaribisha timu ya Dodoma Jiji katika uwanja wa KMC Complex na Coastal Union itakuwa mwenyeji wa timu ya Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga” amesema Mwayela.

“Maandalizi yapo tayari kwa upande wetu kama Bodi ya Ligi na masuala yote ya usimamizi yapo vizuri huku klabu zote 16 zikiendelea kusajili ili kujiimarisha vema tayari kwa msimu mpya. Ratiba hiyo imezingatia matukio mbalimbali ya soka yaliyopo mbele yetu ikiwemo michuano ya kimataifa na kitaifa” ameongeza Mwayela.

Mwayela amesema pamoja na hayo Ligi yetu inatarajiwa kutatamatika mei 23, 2026 ili kuruhusu wachezaji watakaopata nafasi ya kuitwa na timu zao zitakazofanikiwa kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2026.

“Ligi inatarajiwa kutamatika mei 23 ili kuruhusu wachezaji ambao timu zao za taifa zitafuzu Kombe la Dunia kwenda kujiandaa na michuano hiyo na mchezo wa watani wa jadi kati ya Young Africans na Simba ‘Kariakoo Dabi’ mzunguko wa kwanza utapigwa Disemba 13, 2025 huku mchezo wa marudiano ukipigwa April 4” amesema Mwayela.

Aidha ameongeza kuwa ubora waliouonyesha wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani yaani CHAN umetokana na uimara wa Ligi Kuu ya NBC.

PACOME ,HAMDI WABEBA TUZO ZA JUNI LIGI KUU YA NBC.

KIUNGO wa timu ya Young Africans, Peodoh Pacome Zouzoua amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Juni wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2024/2025, huku Miloud Hamdi wa Yanga, akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.
Pacome alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Clatous Chama wa Yanga na Kibu Denis wa Simba, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitatu ambayo Yanga ilicheza mwezi huo akifunga mabao matatu na kuhusika na bao moja kwa dakika 242 alizocheza.

Kwa upande wa Hamdi aliyeingia fainali na Rachid Taoussi wa Azam FC na Fred Felix wa Pamba Jiji, aliiongoza Yanga kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo na kutwaa ubingwa wa wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2024/2025. Yanga ilizifunga Tanzania Prisons (0-5), Dodoma Jiji (5-0) na Simba (2-0).

Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara, Jackson Mwendwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Juni kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB) KUPOKEA MAONI YA MABORESHO YA KANUNI ZA LIGI

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inaujulisha umma kuwa leo Julai 11, 2025 imeanza rasmi kupokea maoni ya maboresho ya Kanuni za Ligi kuelekea msimu wa 2025/2026.

Zoezi hilo la kupokea maoni litafanyika kwa kipindi cha majuma matatu ambapo litafungwarasmi Agosti 1, 2025.

Maoni ya maboresho ya kanuni yawasilishwe TPLB kwa kupitia njia zifuatazo;

i. Barua pepe – maoni@ligikuu.co.tz

ii. Ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) – +255 758 500 222

iii. Kuwasilisha kwa mkono katika ofisi za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania zilizopo ghorofa

ya 14 kwenye jengo la NSSF (Mafao House), Ilala Dar es Salaam.

Bodi inawaomba wadau wote wa Ligi Kuu ya NBC, Ligi ya Championship ya NBC, First League na mpira wa miguu kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya Ligi zetu kwa kuchangia maoni yatakayosaidia kuboresha kanuni zake.

Wadau wanakumbushwa kuwa kanuni bora ndio msingi wa kupatikana kwa ligi bora na maendeleo ya mpira wa miguu kwa ujumla hivyo ushiriki katika zoezi hili ni jambo la muhimu sana.

STAND UNITED, FOUNTAIN GATE NI VITA YA KUCHEZA LIGI KUU YA NBC.

 

HATUA ya mtoano wa nani kusalia ama kupanda Ligi Kuu ya NBC inaendelea kesho kwa mchezo mmoja kati ya Stand United ya mkoani Shinyanga itakayokuwa mwenyeji wa timu ya Fountain Gate kwenye uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

Mchezo huo utakaopigwa saa kumi alasiri utakuwa muhimu kwa timu zote ili kujihakikishia kucheza kwenye ligi namba nne kwa ubora barani Afrika.

Stand United ambao msimu wa 2024/2025 imecheza Ligi ya championship ya NBC inapaswa kupata ushindi wa matokeo ya jumla ya michezo ya nyumbani na ugenini ili kupanda Daraja huku timu ya Fountain Gate nayo ikipaswa kufanya hivyo ili kuhakikisha inabaki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.

Stand imepata nafasi ya kucheza hatua ya mtoano baada ya kuitoa timu ya Geita Gold kwa matokeo ya jumla huku Fountain ikicheza baada ya kupoteza kwenye matokeo ya jumla dhidi ya Tanzania Prisons.

Tatu Malogo kutoka Tanga ndiye mwamuzi atakaesimamia mchezo huo wa kwanza akisaidiwa na Hamdan Said kutoka Mtwara, Zawadi Yusuph kutoka Dar es Salaam na Shija Shurugwai kutoka mkoani Shinyanga.

PRISONS UHAKIKA LIGI KUU NBC 2025/26.

TIMU ya Tanzania Prisons imefanikiwa kusalia Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga timu ya Fountain Gate 3-1 katika mchezo uliochezwa uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Ilimchukua dakika saba mchezaji wa Tanzania Prisons,Beno Ngasa kufungua ukurasa wa mabao huku mchezaji wa Fountain Gate Laurian Makame akisawazisha dakika ya 27 kabla ya Ezekiel Mwashilindi kuiongezea Prisons bao dakika ya 45 hivyo maafande hao Kwenda mapumziko wakiongoza 2-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika ya 47 ya mchezo huo mchezaji wa Prisons Oscar Mwajanga aliongeza bao la tatu kwa timu hiyo na matokeo yakisalia hivyo mpaka mwisho wa mchezo .

Tanzania Prisons wamesalia Ligi Kuu ya NBC kwa uwiano wa mabao 4-2 katika michezo yote miwili ambayo timu hiyo na Fountain Gate zimecheza.