LIGI ya NBC Championship Mzunguko wa 16 leo imeendelea kwa michezo minne ya mwisho ya mzunguko huo iliyochezwa viwanja mbalimbali nchini kuanzia majira ya saa nne asubuhi na saa kumi jioni.
Bigman waliwakaribisha Mbeya City katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi saa nne asubuhi baada ya mchezo huo kuahirishwa kuchezwa jana kutokana na mvua iliyonyesha mkoani Lindi na kusababisha uwanja kujaa maji.
Katika mchezo huo Bigman walifanikiwa kuchukua alama 3 kutoka kwa Mbeya City na kufikisha alama 25 katika msimamo wa Ligi hiyo wakiwa nafasi ya saba baada ya mchezaji wao Francis Kapeta kufunga bao pekee kwa mkwaju wa penati hivyo mchezo kumalizika 1-0.
Mchezo mwingine ulichezwa majira ya saa kumi jioni ambapo timu ya Stand United waliwakaribisha timu ya Kiluvya katika uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.
Dakika ya saba ya mchezo huo Stand United walifungua akaunti ya mabao kupitia mchezaji wao Lukas Sendama na dakika kumi baadae Adam Uledi aliongeza bao la pili hivyo kuwafanya Stand United kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao mawili.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Kiluvya walifanikiwa kupata bao dakika ya 66 ya mchezo huo kupitia mchezaji wao Hassan Bundala na dakika ya 82 Sendama alirudi tena nyavuni hivyo kuwafanya Stand United kuchukua alama zote tatu na mchezo kumalizika kwa 3-1, Stand United wamepanda hadi nafasi ya nne wakiwa na alama 32.
Kwa upande wa mechi ya Mbuni dhidi ya timu ya Polisi Tanzania iliyochezwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha mechi ilianza saa kumi alasiri.
Katika mchezo huo Mbuni walifanikiwa kupata bao dakika ya 33 ya mchezo huo kupitia mchezaji Malulu Thomas kabla ya Hassan Rishedy kuongeza bao la pili dakika ya 44 hivyo Mbuni hivyo matokeo kubaki hivyo hadi mwisho wa mchezo huo 2-0 hivyo kufikisha alama 23 huku wakiwa nafasi ya tisa kakika msimamo.
Timu ya Transit Camp waliwakaribisha timu ya Biashara United kutoka mkoani Mara kwenye uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi Mkoani Pwani
Katika mchezo huo Biashara United walifanikiwa kubeba alama tatu baada ya mchezaji wao Timotheo Abubakar kufunga bao dakika ya 28 ya mchezo huo ambao ulitamatika kwa matokeo ya 0-1 hivyo Biashara kufanikiwa kupata alama tatu mhimu wakifikisha alama 4 huku wakiwa wa mwisho katika msimamo wa Ligi hiyo.
 
					 
		