BAADA ya kuifunga Fountain Gate mabao 4-1 ugenini timu ya TRA imeshinda mchezo wa pili mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga Namungo mabao 2-0 katika uwanja wa Black Rhino uliopo wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Mabao ya Chamou Karaboue na Joseph Akandwanaho yalitosha kuwapa furaha ‘walipa kodi’ huku yakipeleka huzuni na vilio kwa ‘Wauaji wa kusini’ wenyeji wa mkoa wa Lindi..
Chamou aliyesajiliwa na TRA akitokea kwa ‘wababe’ wa Kariakoo timu ya Simba alifunga bao lake la kwanza kwa timu yake huku akipokea pasi ya mwisho kutoka kwa Valentin Nouma aliyekuwa Simba pia ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa mchezo huo akiisaidia kupata alama tatu bila kuruhusu bao.
Mkoani Singida kwenye uwanja wa Airtel Stadium timu ya Singida Black Stars ilishindwa kutamba nyumbani ikikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Simba na kupoteza mchezo wa pili mfululizo nyumbani baada ya kufungwa 3-0 na Young Africans.
Anicet Oura alikuwa wa kwanza kufungua akaunti ya mabao kwa ‘Mnyama’ akitumia vizuri pasi ya kichwa kutoka kwa Allasane Kante bao ambalo lilifutika dakika chache kabla ya mapumziko baada ya Ndumumwe Mossi kuisawazishia Singida.
Dakika tano kabla ya dakika 90 kukamilika Elie Mpanzu aliyeingia akitokea benchi alitumia vizuri pasi ya mchezaji bora wa mchezo huo Clatous Chama na kuiandikia Simba bao la pili lililohakikisha alama tatu muhimu kwa ‘Mnyama’ zilizomfanya kufikisha alama 27 na kutia kambi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo wa mwisho ulishuhudia ‘matajiri wa chamazi’ timu ya Azam ikiishushia kipigo timu ya Dodoma jiji kwa mabao 3-0 kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma na kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo huo ulioshuhudia kiungo Feisal Salum akifunga bao moja na kutoa pasi ya bao baada ya kurejea uwanjani akitoka kutumikia adhabu aliyopewa baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Pamba Jiji.
Mabao mengine yalifungwa na mchezaji wa zamani wa Dodoma Zidane Sereri aliyekuwa mwiba mkali kwa ‘walima zabibu’ na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mchezo huo akiingia kambani mara mbili.