Timu ya Yanga imeendeleza ubabe Ligi Kuu ya NBC kwa kucheza michezo sita bila kupoteza hivyo kufikisha alama 18 na kuwa nafasi ya pili katika msimamo ikiwa nyuma ya Singida Black Stars kwa alama moja.
Yanga jana iliifunga timu ya JKT Tanzania kwa mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa jana uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga yalifungwa na wachezaji Pacome Zouzoua ambaye pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kiungo Mshambuliaji wa timu hiyo Clatous Chama ambae pia alitoa asisti ya goli ya goli la kwanza.
Aidha katika mchezo huo kipa wa JKT Tanzania,Dennis Richard alipewa kadi nyekundu baada ya kuucheza mpira kwa mikono akiwa nje ya box hivyo kuifanya JKT kufanya mabadiliko kwa kumtoa Hassan Kapalata na kumuingiza mlinda mlango Omary Gonzo .
Ligi kuu ya NBC inaendelea leo kwa mchezo mmoja utakaochezwa mkoani Tabora ikizikutanisha timu za Tabora United na Pamba Jiji kutoka jijini Mwanza.