MTINE, POPAT WAFUNGUKA SEMINA YA FIFA UENDESHAJI KLABU NCHINI.

Watendaji Wakuu wa Klabu za Yanga na Azam wameshukuru Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wakishirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Pamoja na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa kuandaa semina ya siku mbili jijini Dar es salaam kuhusu Weledi katika Uendeshaji wa klabu nchini kwa Watendaji Wakuu na Wenyeviti wa Klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC.

Akizungumza katika semina hiyo Mtendaji Mkuu wa Yanga Andre Mtine amesema kuwa semina hii ni muhimu kwani elimu haina mwisho na itawezesha viongozi wa klabu kutambua namna nzuri ya kuendesha klabu.

“Elimu ni jambo la muhimu kwa kila mtu na haina mwisho iwe kijana ama mzee bado anapaswa kujifunza hii ni nzuri kwetu kwani tunajifunza namna ya kuendesha klabu zetu kwa manufaa ya Ligi yetu ya NBC” Alisema Mtine.

Kwa upande waka Mtendaji Mkuu wa Azam Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema kuwa anashukuru kwa kupata fursa hii adimu kutoka FIFA wakishirikiana na TFF Pamoja na Bodi ya Ligi kwani itawajengea ujuzi na uzoefu mpya kwenye tasnia ya mpira.

“Nashukuru FIFA, TFF na Bodi ya Ligi kwa kuja na semina hii kwani ni fursa adimu naamini itatujengea uwezo na kutupa ujuzi mpya sisi kama watendaji wakuu wa klabu za Ligi Kuu ya NBC na kama Azam tunaahidi kwenda kufanyia kazi tulichojifunza na tutaenda kuwafundisha waliopo chini yetu ili nao wanufaike na haya”alisema Popat.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *