TABORA, COASTAL HAKUNA MBABE, AZAM IKITAMBA.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea jana kwa michezo miwili iliyochezwa katika mikoa ya Tabora na Dar es Salaam.

Mchezo uliochezwa mkoani Tabora timu ya Tabora United iliikaribisha timu ya Coastal Union katika mchezo uliochezwa saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na kutamatika kwa sare ya 1-1.

Coastal Union ilianza kufunga bao kupitia kwa mchezaji Jeremiah Ntambwe aliyefunga katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na alikuwa mchezaji wa Tabora, Banele Sikhondze aliyefanikiwa kuweka sawa mzani baada ya kuipatia bao timu yake hivyo kufanya ubao kusomeka 1-1 mpaka mwisho wa mchezo huo.

Golikipa wa Tabora Hussein Masalanga alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na namna alivyoweza kulinda lango lake dhidi ya mashambulizi yaliyofanywa na Coastal Union.

Mchezo wa pili ulikuwa kati ya Azam na Fountain Gate kwenye uwanja wa Azam Complex na kumalizikwa kwa Azam kushinda kwa mabao 2-0.

Gibril Sillah ndio alianza kutikisa nyavu za Fountain Gate dakika ya 40 ya mchezo huo akipokea pasi kutoka kwa kiungo wa timu hiyo Feisal Salum hivyo kuwafanya Azam kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja.

Kocha wa Azam Rachid Taoussi alifanya mabadiliko kipindi cha pili cha mchezo huo na kumtambulisha mchezoni mshambuliaji Allasane Diao ambaye amerejea baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha aliyokuwa nayo.

Allasane aliiongezea bao timu yake hivyo kuifanya Azam kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya kufikisha alama 33 na Kiungo wa Azam Feisal Salum alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa mchezo mmoja utakaochezwa uwanja wa KMC Complex kati ya Simba na KenGold kutoka jijini Mbeya saa 10:00 alasiri.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *