MZUNGUKO wa 21 wa Ligi Kuu ya NBC unaanza leo rasmi ambapo michezo miwili itachezwa katika viwanja vya Sokoine jijini Mbeya na Meja Jenerali Isamuhyo mkoani Dar es Salaam.
Katika mchezo utakaochezwa majira ya saa nane mchana, timu ya Tanzania Prisons ‘wajelajela’ watakuwa wenyeji wa Tabora United ikiwa ni mchezo wa duru ya pili.
Tanzania Prisons ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imefunga mabao 11 na kuruhusu mabao 25 katika michezo 20 iliyocheza mpaka sasa na ikikusanya alama 17.
Tabora United ipo nafasi ya tano kwenye msimamo na imefunga mabao 24 na kuruhusu mabao 25 huku ikivuna alama 33 katika michezo 20 iliyocheza mpaka sasa.
Mchezo wa pili utachezwa uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo mbweni Dar es Salaam ‘wazee wa kichapo cha kizalendo’ wataikaribisha timu ya ‘wanankurukumbi’ kutoka misenyi Kagera.
JKT Tanzania ipo nafasi ya nane katika msimamo huku ikiwa imekusanya alama 23 ikifunga mabao 13 na kufungwa mabao 15.
Kagera Sugar ipo nafasi ya 15 ikiwa imekusanya alama 15 ikifunga mabao 16 ikiruhusu mabao 28 katika michezo 20 waliyocheza mpaka sasa.