IKISALIA mizunguko saba kutamatika kwa Ligi Kuu ya NBC ‘Mlinda lango’ wa timu ya Simba Moussa Pinpin Camara ameendelea kushikilia usukani wa vinara ambao hawajaruhusu mabao kwenye ligi hiyo.
Camara hadi sasa amefikisha idadi ya michezo 15 aliyocheza bila kuruhusu nyavu zake kuguswa huku timu yake ikifungwa mabao nane pekee hadi sasa.
Golikipa huyo wa Simba amemzidi michezo minne mpinzani wake Djigui Diarra wa Yanga anayemfuatia kwa karibu akiwa amekusanya jumla ya michezo 11 bila kuruhusu bao.
Patrick Munthali wa timu ya Mashujaa iliyoruhusu mabao 28 hadi sasa anashika nafasi ya tatu akiwa na michezo 10 bila kuruhusu bao huku idadi hiyo ikiwa sawa na golikipa wa Azam Mohammed Mustapha huku Azam ikiruhusu mabao 12 hadi sasa ikisalia na michezo saba kutamatisha msimu.