LIGI ya Championship ya NBC inazidi kushika kasi ikiwa ni mzunguko wa 24 huku timu nyingi zikionyesha uwezo ambapo kila timu inataka kufuzu kwenda Ligi Kuu ya NBC msimu 2025-26 huku timu za Mtibwa Sugar, Mbeya City, Geita Gold, Mbeya Kwanza na Songea United zikiwa hazijapoteza mchezo wowote nyumbani hadi sasa.
Mtibwa Sugar ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo ikiwa na alama 57 ikicheza michezo 12 kwenye uwanja wake wa Manungu Complex na kufanikiwa kushinda michezo yote.
Mbeya City iko nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ikishinda michezo tisa na kupata sare tatu katika michezo 12 waliyocheza uwanja wao wa nyumbani.
Geita Gold ipo nafasi ya nne katika msimamo ikishinda michezo 11 na kupata sare mchezo mmoja katika michezo 12 iliyocheza ikiwa uwanja wao wa Nyankumbu.
Mbeya Kwanza ipo nafasi ya sita katika msimamo ikicheza michezo 11 nyumbani ikishinda michezo saba na kupata sare michezo minne.
Songea United ipo nafasi ya nane katika msimamo ikicheza michezo 10 nyumbani na kushinda michezo sita huku ikipata sare michezo minne na kukamilisha idadi ya timu ambazo hadi sasa hazijapoteza mchezo wowote nyumbani.