VINARA wa Ligi Kuu ya NBC Young Africans imeendelea kugawa ‘dozi’ inapocheza uwanja wa ugenini baada ya kuifunga Tabora United mabao 3-0 kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora.
Mchezo wa jana umeshuhudia wachezaji wa Young Africans Prince Dube na Clement Mzize wakifunga bao moja kila mmoja na wote kufikisha mabao 11 msimu huu huku Israel Mwenda akifunga bao la pili msimu huu.
Huu ni mchezo wa tatu mfululizo kwa Young Africans kushinda ugenini baada ya kuifunga Mashujaa 5-0 kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na Pamba JIji 3-0 kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kwenye michezo hiyo Young Africans imefanikiwa kufunga mabao 11 na kufikisha jumla ya mabao 61 huku ikiwa imeruhusu mabao tisa na kuwa timu ya pili kuruhusu mabao machache msimu huu nyuma ya Simba iliyoruhusu mabao nane pekee.