IKICHEZA mchezo wa tano mfululizo timu ya Pamba Jiji imeshindwa kupata ushindi baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na timu ya Namungo kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Namungo ilikuwa ya kwanza kufungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Jacob Massawe huku Pamba ikisawazisha kupitia kwa Nyota Abdoullaye Camara anayecheza kwa mkopo kutokea timu ya Singida Black Stars huku likiwa bao lake la pili msimu huu.
Matokeo hayo yanaifanya Pamba kushuka kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC hadi nafasi ya 13 ikiwa juu ya mstari wa kushuka daraja kwa tofauti ya alama tano.
Namungo imepanda hadi nafasi ya 12 baada ya kupata alama moja na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-26 chini ya kocha Juma Mgunda aliyewahi kufundisha timu za Coastal Union na Simba.