LIGI ya Championship ya NBC imeendelea kwa mzunguko wa 28 ambapo Mtibwa Sugar inaongoza kwa kushinda mechi iliyocheza nyumbani katika uwanja wa Manungu Complex ikishinda mechi zote 14, huku ikifanikiwa kupanda daraja kwenda Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 67 hadi sasa.
Geita Gold imeshinda michezo 13 iliyocheza uwanja wa nyumbani wa Nyankumbu huku timu hiyo ikishika nafasi ya nne baada ya kukusanya alama 54.
Nafasi ya tatu inashikwa na Stand United iliyoshinda michezo 12 katika uwanja wa Kambarage uliopo mkoani Shinyanga ikishika nafasi ya tatu pamoja na kukusanya alama 59.
Mbeya City imefanikiwa kushinda michezo 10 katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya huku ikiwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Championship ikikusanya alama 62 sawa na TMA iliyoshinda michezo 10 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.
Kwa upande wa timu ya Bigman iliyopo nafasi ya saba kwenye msimamo ikiwa na alama 46 ikiwa imeshinda michezo tisa katika uwanja wa Ilulu uliopo mkoani Lindi.
Mbeya Kwanza na Songea United zimefanikiwa kushinda michezo nane kila timu katika viwanja vyao vya nyumbani ambavyo ni Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kwa upande wa Mbeya Kwanza na Majimaji mkoani Songea kwa upande wa Songea United.