MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba, Steven Mukwala amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wamwezi Mei wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2024/25, huku Fadlu Davids akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.
Mukwala alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Jean Charles Ahoua pia wa Simba na Jafari Kibaya wa Mashujaa, alioingia nao fainali katika mchakato waTuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF).
Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo minne aliyocheza mwezi huo na kufunga mabao matatu na kuhusika na lingine moja kwa dakika 233 alizocheza.
Kwa upande wa Fadlu aliyeingia fainali na Miloud Hamdi wa Yanga na Rachid Touassi wa Azam, aliiongoza Simba kushinda michezo yote mitano iliyocheza mwezi huo na
kuendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi. Simba ilizifunga Singida Black Stars (1-0), KMC (1-2), Pamba Jiji (5-1), Mashujaa (2-1) na JKT Tanzania (0-1).
Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Ashraf Omar kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Mei kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.
Wakati huohuo Kamati ya Tuzo za TFF, imemchagua Frank Edmund Rutha wa African Sports kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Mei wa Ligi ya NBC Championship 2024/25, huku Malale Hamsini wa Mbeya City akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Frank aliyeingia fainali na Kilaza Mazoea na Eliud Ambokile wote wa Mbeya City,alionesha kiwango kizuri ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne kwa dakika 170 alizocheza za michezo miwili.
Kwa upande wa Malale aliyeingia fainali na Kessy Abdallah wa African Sports na Abdul Mingange wa Songea United, aliiongoza timu yake kushinda michezo yote miwili iliyocheza na kuiwezesha kupanda Ligi Kuu ya NBC msimu 2025/2026.