TIMU ya KenGold imeshindwa kutamba nyumbani kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora baada ya kufungwa na timu ya Simba mabao 0-5 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Ilimchukua dakika 20 mchezaji wa Simba Kibu Denis kufungua ukurasa wa mabao huku Ellie Mpanzu akiongeza bao la pili dakika ya 22 ya mchezo huo na dakika ya 25 Kibu Denis alirejea tena nyavuni kuongeza bao la tatu kwa timu yake na kuifanya kuwa mbele kwa mabao matatu.
Dakika ya 36 ya mshambuliaji wa Simba Leonel Ateba aliiongezea timu yake bao la nne na kufanya mchezo huo Kwenda mapumziko ubao ukisomeka 0-4.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu ya KenGold kujaribu kusaka mabao ili kuweka mzani sawa lakini dakika ya 75 mchezaji wa Simba Jean Ahoua aliongeza bao kwa timu yake hivyo mchezo kutamatika kwa ubao kusomeka 0-5.
Kibu Dennis aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo huku Jean Ahoua akiongeza wigo wa mabao akifikisha bao la 16 msimu huu na kuendelea kushikilia usukani wa vinara mabao.