PACOME ,HAMDI WABEBA TUZO ZA JUNI LIGI KUU YA NBC.

KIUNGO wa timu ya Young Africans, Peodoh Pacome Zouzoua amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Juni wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2024/2025, huku Miloud Hamdi wa Yanga, akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.
Pacome alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Clatous Chama wa Yanga na Kibu Denis wa Simba, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitatu ambayo Yanga ilicheza mwezi huo akifunga mabao matatu na kuhusika na bao moja kwa dakika 242 alizocheza.

Kwa upande wa Hamdi aliyeingia fainali na Rachid Taoussi wa Azam FC na Fred Felix wa Pamba Jiji, aliiongoza Yanga kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo na kutwaa ubingwa wa wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2024/2025. Yanga ilizifunga Tanzania Prisons (0-5), Dodoma Jiji (5-0) na Simba (2-0).

Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara, Jackson Mwendwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Juni kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

2 comments

Join the Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *