Transit VS Kagera

NI VITA YA NAFASI NBC CHAMPIONSHIP LEO

LIGI ya Championship ya NBC inaendelea leo kwa michezo miwili mikubwa yenye uzito wa kipekee katika kupambania nafasi za juu na kuepuka hatari ya kushuka daraja.

Katika mchezo unaovuta hisia za mashabiki wengi, Transit Camp itaialika Kagera Sugar kwenye uwanja wa Filbert Bayi mkoani Pwani, huku mchezo mwingine ukizikutanisha Hausung na African Sports katika uwanja wa Amani, mkoani Njombe.

Transit Camp inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na alama 33, inaingia uwanjani ikiwa na lengo moja tu la ushindi na kukusanya alama tatu zitakazoiwezesha kufikisha jumla ya alama 36 na kupanda hadi nafasi ya pili, ikinufaika na faida ya matokeo ya ana kwa ana (head to head) dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa upande wao, Kagera Sugar waliopo nafasi ya pili wakiwa na alama 36, wanahitaji ushindi ili kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC, wakisubiri pia kwa jicho la pili matokeo ya mchezo wa Geita Gold dhidi ya Barberian unaotarajiwa kuchezwa kesho.

Ushindani wa alama na nafasi baina ya timu hizo mbili unaipa mechi hiyo hadhi ya ushindani wa kweli, ikitarajiwa kuwa miongoni mwa michezo inayofuatiliwa kwa karibu zaidi leo, hasa kutokana na ubora wa vikosi na mwenendo wao katika michezo ya hivi karibuni.

VITA YA KUBAKI LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC

Wakati huo huo, vita nyingine ya kusaka uhai itapigwa Njombe, ambapo Hausung na African Sports zitavaana katika pambano la kujiokoa dhidi ya mstari wa kushuka daraja huku timu zote mbili zikikusanya alama nane na zikitofautiana tu katika idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Ushindi kwa Hausung (nafasi ya 14) au African Sports (nafasi ya 15) utaifanya timu husika kupaa hadi nafasi ya 13 hatua muhimu katika mbio za kusalia Ligi ya Championship ya NBC.

Mchezo wa Transit Camp dhidi ya Kagera Sugar utarushwa mubashara (Live) kupitia chaneli ya FIFA+, kuwapa fursa mashabiki wengi kushuhudia moja ya michezo mikubwa ya msimu huu.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *