LIGI Kuu ya NBC imeendeleza burudani ya aina yake huku mashabiki wakishuhudia ushindi mwembamba wa bao moja kwa Singida Black Stars dhidi ya Coastal na sare ya kusisimua ya mabao 2-2 kwa Pamba Jiji dhidi ya Azam FC.
Katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa airtel mkoani singida, Singida Black Stars waliikaribisha Coastal union na iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union huku shujaa wa mchezo huo akiwa mshambuliaji Joseph Guede aliyefunga bao pekee dakika ya 72 kwa umakini mkubwa akimalizia shambulizi lililowapa furaha mashabiki wa Singida.
Coastal walijitahidi kusaka bao la kusawazisha lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Singida ulihakikisha wanatoka bila alama wala bao.
Wakati huo huo jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba saa kumi kamili jioni kulishuhudiwa pambano kali kati ya Pamba Jiji FC na Azam lililomalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Pamba Jiji walianza kuonyesha makali kwa bao la Himid Mao aliyejifunga dakika ya 45 kabla ya John Nakibinge kuongeza la pili dakika ya 48.
Hata hivyo Azam hawakukata tamaa wakarejea kwa nguvu kupitia Jean Ngita dakika ya 56 na baadaye Feisal Salum kufunga kwa penalti dakika ya 59 na kuifanya mechi kuwa ya kusisimua hadi dakika ya mwisho.
Mchezo huo ulishuhudia Feisal akionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea mchezaji wa Pamba rafu mbaya na hivyo feisal kukosa mchezo unaofuata wa Dar es Salaam derby utakaoikutanisha Azam dhidi ya Young Africans.
Kwa matokeo hayo, Singida Black Stars wanaondoka na alama tatu muhimu, huku Azam na Pamba Jiji wakigawana alama mojamoja.