Tulihesabu miezi, tukahesabu wiki, tukahesabu siku na sasa tunahesabu masaa kuelekea mchezo mkubwa wa Kariakoo Derby kati ya Young Africans SC na Simba SC utakaopigwa katika dimba la Amaan, visiwani Zanzibar kwenye mpambano wa kusisimua utakaochezwa kuanzia majira ya saa 2:15 usiku leo Machi Mosi.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu ya NBC kwa Kariakoo Derby kuchezwa visiwani Zanzibar huku likiwa tukio la kipekee linaloandika ukurasa mpya wa soka la Tanzania, Swali linalobaki ni moja tu nani ataanza kuandika historia hiyo kwa ushindi?
Young Africans SC wanaingia katika pambano hili wakiwa kileleni na alama 28 baada ya michezo 10 wakishinda michezo tisa na kutoka sare mchezo mmoja pekee huku Safu yao ya ushambuliaji ikiwa moto wa kuotea mbali, wakifunga jumla ya mabao 28 idadi kubwa kuliko timu yoyote hadi sasa.
Siyo hilo tu, bali pia wameonyesha uimara wa kipekee katika safu ya ulinzi kwa kuruhusu mabao mawili pekee, rekodi bora zaidi msimu huu.
Lakini kwa upande wa Simba SC, ‘Wekundu wa Msimbazi’ wamejikusanyia alama 23 katika michezo 10 na wakishinda michezo saba, wakipoteza mmoja na kutoka sare mmoja, wakifunga mabao 18, wanashika nafasi ya pili kwa ufungaji nyuma ya watani zao na safu yao ya ulinzi pia imeonyesha uthabiti kwa kuruhusu mabao manne pekee, wakibaki miongoni mwa timu zenye safu imara zaidi ya ulinzi.
Hadi sasa, ni Young Africans SC na Azam FC pekee ambao hawajapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu. Je, Simba SC wataweza kuivunja rekodi hiyo na kuandika sura mpya ya Derby ya kwanza visiwani Zanzibar?
Leo usiku, historia itaandikwa. Swali ni itaandikwa kwa wino wa nani ‘Wananchi’ Young Africans au ‘wekundu wa Msimbazi’ Simba SC ?
Tukune Amaan Stadium saa 2:15 usiku tuzishuhudie ladha za Ligi namba 6 kwa ubora barani Afrika na 54 Duniani, Ligi Kuu ya NBC.