BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inautaarifu umma kuwa mchezo namba saba (7) wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 (TRA United FC vs Simba SC), utafanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Aprili 9, 2026 kuanzia saa 10:00 alasiri.
Aidha, Bodi inatoa taarifa kuwa mashabiki wote ambao walinunua tiketi kwa ajili ya mchezo huo ambao uliahirishwa Machi 14, 2026 baada ya mvua kubwa kunyesha jijini Arusha na kusababisha uwanja kukosa sifa za kisheria, watatumia tiketi hizo kuingia uwanjani katika mchezo wa Aprili 9, 2026, ambapo shabiki atalazimika kuwa na kadi (N-CARD) ambayo aliitumia kununua tiketi ya mchezo ulioahirishwa, kwa ajili ya uhakiki getini.
Tayari wauzaji wa tiketi za mchezo huo, National Internet Data Center (NIDC) wamerejesha tiketi zote zilizonunuliwa, kwenye kadi za mashabiki hao bila kujali shabiki alikuwa ameshaingia uwanjani ama hakuingia kabisa, na kwamba mashabiki hao hawatapaswa kununua tena tiketi.Tiketi ambazo ziliuzwa katika mchezo huo ni VVIP 95, VIP 567 na Mzunguko 3,215.
Bodi inawakumbusha mashabiki ambao hawakununua tiketi kwenye mchezoulioahirishwa, kuwa tiketi zinapatikana (zinauzwa) kwenye vituo vya N-CARD vya kuuzia tiketi na kupitia mitandao ya simu kwa gharama zifuatazo; VVIP – 50,000, VIP (Wing A & B) – 30,000 na Mzunguko – 10,000
Bodi ya Ligi inawashukuru sana mashabiki wa mpira wa miguu kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa Bodi na klabu zake, ikiwemo kununua tiketi na kuingia viwanjani kuziunga mkono klabu zetu.
Imetolewa na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)