LIGI Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo miwili itakayopigwa kwenye viwanja vya Airtel mkoani Singida ambapo Singida Black Stars itaialika KMC na CCM Kirumba mkoani Mwanza timu ya Pamba Jiji itaikaribisha timu ya Young Africans.

Michezo hiyo ni muhimu kwa timu zote kutokana na namna Ligi hiyo inavyozidi kupamba moto, Singida Black Stars iliyopo nafasi ya sita inacheza majira ya saa nane mchana huku ikiwa imeshinda michezo saba sare nne na kufungwa michezo sita huku ikikusanya alama 25.

Kwa upande wa KMC inashika nafasi ya mwisho (16) katika msimamo ikicheza michezo 17 na kushinda miwili, sare mbili na kufungwa 13 huku ikikusanya alama 8.

Mchezo wa pili ni muhimu kwa Pamba Jiji ikitaka kuendeleza rekodi ya kutokufungwa mchezo wowote katika uwanja wao wa nyumbani katika michezo tisa timu hiyo imeshinda michezo mitano na sare nne huku Young Africans ikitaka kuendeleza kukusanya alama ili iwe katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC.
Pamba ambayo iPo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC imecheza michezo 17 ikishinda michezo sita sare nane na kufungwa michezo mitatu huku ikiweza kukusanya alama 26.

Kwa upande wa Young Africans ipo nafasi ya kwanza katika msimamo ikiwa imecheza michezo 17 kushinda michezo 12 na sare tano huku ikiwa imekusanya alama 41.