SIMBA, COASTAL ZAGAWA ‘DOZI’ LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo iliyochezwa katika mikoa miwili tofauti ambapo Simba ilikuwa ugenini dhidi ya Fountain gate mchezo uliochezwa uwanja wa Sheikh Abeid mkoani Arusha na ‘Mnyama’ kusibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Simba walidhibiti mchezo kuanzia mwanzo hadi mwisho wakionyesha ubora mkubwa wa kushambulia na bao la kwanza lilifungwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza na Clatous Chama ambaye aliwapa Simba mwanzo mzuri.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi Libase Gueye akiongeza bao la pili dakika ya 53 akitumia vizuri pasi ya Selemani Mwalimu.

Bao la tatu kilifungwa dakika ya 71 kwa mchezaji wa Fountain Gate Shaban Mgunda kujifunga baada ya kushindwa kuokoa krosi iliyopigwa na Elie Mpanzu.

Ushindi huu unaimarisha nafasi ya Simba katika msimamo wa ligi kuu wakiwa nafasi ya Pili na alama 39 huku Fountain Gate wakiendelea kupambana kujinasua katika eneo hatari wakiwa nafasi 14 baada ya kukusanya alama 16.

Mchezo wa Pili Coastal union iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Dodoma jiji kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Coastal union ilifungua ukurasa wa mabao dakika ya 15 kupitia kwa Greyson Gwalala kwa shuti kali kabla ya Maabad Maulid kuongeza bao la pili dakika ya 32 na kuwapa wenyeji uongozi mzuri wa 2-0 kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilishuhudia ushindani ukiendelea huku Dodoma jiji wakijitahidi kurejea mchezoni na matumaini yalirejea baada ya kupata bao dakika ya 90+1 kupitia kwa Waziri Junior ambalo lilidumu kwa dakika tatu pekee kabla ya Geofrey Manyac kuzima matumaini ya Dodoma kusawazisha bao kwa kuandika la tatu kwa Coastal.

Ushindi huo unaifanya Coastal union kufikisha alama 19 wakikwea hadi nafasi ya 12 huku Dodoma wakisalia na alama 24 kwenye nafasi ya nane.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *