LIGI ya Championship ya NBC msimu wa 2025/26 imezidi kupamba moto huku ushindani ukiwa mkali katika kila kona ya msimamo, wakati mzunguko wa 22 ukielekea kufungwa rasmi.
Vinara Geita Gold wameendelea kuthibitisha ubora wao baada ya kuichapa Hausung mabao 6-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita huku ushindi huo wa kishindo ukiifanya Geita Gold kufikisha alama 55 baada ya michezo 22, wakizidi kujikita kileleni.
Wanaowafuatia kwa karibu ni majirani zao wa Kagera Sugar ambao hawakuachwa nyuma baada ya kupata ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya B19 wakifikisha alama 52 na kuendelea kuweka presha kwa vinara Geita.
Katika mchezo mwingine, Mbeya Kwanza waliendeleza ubora wao wakiwa ugenini kwa kuichapa Kengold mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya, ushindi unaoifanya Mbeya Kwanza kujikita katika nafasi ya tatu kwa alama 48 wakiendelea kusalia kwenye mbio za kupanda daraja.
Nayo Polisi Tanzania ilionyesha uthabiti baada ya kuibuka na ushindi mgumu wa mabao 2-1 dhidi ya Transit Camp, ushindi uliowapandisha hadi nafasi ya nne wakifikisha alama 45.
Msimamo wa ligi kwa sasa unaonyesha vita kali, ambapo timu tano za juu zinaendelea kuwania nafasi za kupanda daraja moja kwa moja au kushiriki michezo ya mtoano (playoffs) huku Kila alama ikiwa na thamani ya dhahabu kadri ligi inavyoingia hatua za mwisho.
Hata hivyo, hali ni ya wasiwasi kwa timu za chini ya msimamo, Hausung na Barberian wanaoshika nafasi ya 15 na 16 wapo kwenye hatari kubwa ya kushuka daraja iwapo hawatabadilisha mwenendo wao haraka.
Mzunguko wa 22 unatarajiwa kukamilika leo kwa pambano kati ya Gunners na Mbuni litakalopigwa Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro kuanzia saa 10:00 jioni.