KWENYE msimu huu wa Ligi Kuu ya NBC klabu ya Young Africans imejijengea heshima kubwa si tu kwa kushinda michezo yake bali namna inavyoshinda kwa mabao mengi na soka la kuvutia linaloacha alama kwa mashabiki na wapinzani wao.
Katika msimu huu, Young Africans imeonyesha ubora wa kipekee kwenye safu ya ushambuliaji kwa kutoa vipigo vizito kwa baadhi ya timu za Ligi Kuu ya NBC.
Moja ya matokeo yaliyotikisa ni ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa ya Kigoma iliyoupata kwenye uwanja wa KMC, ambapo walionesha tofauti kubwa ya kiwango kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo ikiwa hadi kufika mapumziko ‘Wananchi’ walikuwa wanaongoza mabao matatu na kipindi cha pili kufunga matatu pia.
‘Mvua’ hiyo ya mabao ilishushwa na Mohamed Damaro, Duke Abuya, Pacome Zouzoua, Prince Dube, Mudathir Yahya na Laurindo Dilson huku golikipa aliyekuwa langoni Abutwalib Mshery akimaliza mchezo bila kuruhusu bao.
Bado ‘Wananchi’ waliongeza ushindi mwingine mkubwa wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania, wakithibitisha kuwa ushindi wao mkubwa si tukio la bahati mbaya bali ni sehemu ya utambulisho wao msimu huu huku kila mchezo ukionekana kama fursa ya kuonyesha ubora zaidi, na Young Africans imekuwa ikipeleka presha kubwa kwa timu pinzani kwa mtindo wao wa kucheza soka la kasi, pasi nyingi, na umaliziaji mkali.
Katika ushindi huo Mohamed Hussein, Prince Dube, Laurindo Dilson, Mudathir Yahya na Sheikhan Hamis waliingia kambani na kupeleka kilio kwa timu ya Mashujaa.
Kana kwamba haitoshi, walirudia tena matokeo ya 6-0 dhidi ya Mbeya City, wakionyesha ukali kwenye ushambuliaji ambapo katika mechi hiyo, mfumo wa timu ulifanya kazi kwa ufanisi mkubwa kuanzia kiungo kinachotengeneza nafasi hadi washambuliaji wanaomalizia kwa umakini wa hali ya juu.
Pacome Zouzoua na Prince Dube walifunga mabao mawili kila mmoja huku Maxi Nzengeli na Mohamed Hussein wakifunga bao moja kila mmoja na kuendelea kuzamisha jahazi la Mbeya City iliyopo kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Kinachovutia zaidi ni namna timu hii imeweza kudumisha njaa ya ushindi licha ya kuwa tayari kileleni mwa msimamo na wachezaji wao wanaonekana kuwa na maelewano mazuri uwanjani, jambo linalochangia kupatikana kwa nafasi nyingi za kufunga katika kila mchezo.
Kwa mashabiki, haya si matokeo tu bali ni burudani, ambapo mabao mengi yanakuwa sehemu ya furaha ya mashabiki walioko uwanjani na wale wanaofuatilia kupitia runinga ikiwa wazi kuwa msimu huu, Young Africans haichezi tu kushinda bali pia kutoa ujumbe kwa wapinzani wao.