Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

TAARIFA YA KAMATI YA UENDESHAJI NA USIMAMIZI WA LIGI YA BODI YA LUGI KUU TANZANIA (TPLB).

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Aprili 18, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba 07: TRA United FC 0-0 Simba SC

Klabu za TRA United na Simba za Dar es Salaam zimetozwa faini Sh. 5,000,000 (milioni tano) kila moja kwa kosa la walinzi wa klabu hizo (Stewards) kupigana mara baada ya timu hizo kuwasili kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi Namba 132: Pamba Jiji FC 0-3 Young Africans SC

Mchezaji Mudathir Yahya wa klabu ya Young Africans amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji, Ibrahim Abraham wakati mchezo unaendelea kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mechi Namba 146: Coastal Union FC 1-1 Mtibwa Sugar FC

Klabu ya Coastal Union ya mkoani Tanga imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la mashabiki wake kurusha chupa za maji kiwanjani wakati mwamuzi wa kati na mwamuzi msaidizi namba moja wakiwa wanatuliza vurugu zilizokuwa zikiendelea baada ya mchezaji wa Mtibwa Sugar, Victor Collins kumsukuma mchezaji wa Coastal Union Athuman Makambo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Mechi Namba 151:  TRA United 2-0 Singida BS

Klabu ya Singida BS ya mkoani Singida imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la viongozi wake wawili kuingia kiwanjani na kumwaga vimiminika. Viongozi hao walifanya tukio hilo lililotafsiriwa kama vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina, kabla ya timu kutoka kwa ajili ya kupasha moto misuli.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi Namba 152: Azam FC 0-0 Simba SC

Klabu ya Azam ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la viongozi wa benchi la ufundi pamoja na wachezaji kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:21 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo na makubaliano yaliyofanyika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo huo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Klabu ya Simba ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi) kwa kosa la mashabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wa mchezo huo, mara baada kunyoosha kibendera kuashiria mchezaji wa Simba kuotea.

Hili ni kosa la kujirudia kwa klabu ya Simba ambapo ndani ya msimu huu wa Ligi kuu ya NBC 2025/2026, mashabiki wa klabu hiyo walitenda kosa hilo katika michezo miwili tofauti na kusababisha klabu kuadhibiwa.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Imetolewa na;

 

Idara ya Habari na Mawasiliano

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)

Aprili 20, 2026

 

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *