SAFARI inaanza Aprili 29, visiwani Zanzibar ambapo macho yote yataelekezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex timu za Simba na Young Africans (Yanga) zitakapokutana katika fainali ya Kombe la Muungano kwenye mchezo wenye uzito wa kipekee unaobeba heshima ya kitaifa na hadhi ya ushindani wa kihistoria kati ya timu hizi mbili.
Fainali hii si tu pambano la kutwaa taji, bali ni kipimo cha nguvu, mbinu na utayari wa kila kikosi kuelekea mechi nyingine kubwa zaidi inayofuata ya Ligi Kuu ya NBC timu hizo zitakapokutana.
Ndani ya dakika 90 (au zaidi), mshindi atajipatia faida ya kisaikolojia itakayoweza kuathiri moja kwa moja matokeo ya Kariakoo derby ya Mei 3 kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam unaotumiwa na timu ya Simba.
Kabla ya Kariakoo Derby ya Mei 3 ndani ya Dar es Salaam, hali ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC inaipa hadithi hii uzito wa kipekee kuelekea mchezo huo ambapo Yanga wanaongoza wakiwa na rekodi ya kuvutia.
‘Wananchi’ wamecheza michezo 19 bila kupoteza wakishinda 14, sare tano, mabao 44 ya kufunga na mabao matatu tu ya kufungwa huku ikikusanya alama 47 hadi sasa.
Kwa upande wa ‘Mnyama’ ameshinda 12, sare sita, ‘kichapo’ kimoja dhidi ya Azam, mabao 32 ya kufunga na saba ya kuruhusu huku ikikusanya jumla ya alama 42 hadi sasa.
Takwimu hizi zinaonyesha tofauti ndogo sana kwa ‘miamba’ hii inayotikisa Ligi Kuu ya NBC msimu huu huku Yanga wakionekana kuwa na uimara mkubwa hasa kwenye safu ya ulinzi na Simba wakibaki kuwa tishio lenye uwezo wa kubadilisha mchezo kwa haraka kwenye safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa na Selemani Mwalimu.
Katika upande wa ushambuliaji, Yanga wanaonekana kuwa na mgawanyo mpana wa mabao, hali inayowafanya kuwa vigumu kuzuilika huku wachezaji wao Prince Dube raia wa Zimbabwe akifunga mabao nane, Pacome Zouzoua wa Ivory Coast akifunga saba na Mudathir Yahya raia wa Tanzania akifunga saba huku akitarajiwa kukosa mchezo huo wa jumapili kutokana na adhabu aliyopewa ya kufungiwa baada ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji Ibrahim Abraham.
Kwa upande wa ‘Mnyama’ mchezaji wa Wydad Casablanca ya Morocco raia wa Tanzania anayekipiga kwenye timu hiyo kwa mkopo Selemani Mwalimu hadi sasa amefunga mabao 6 huku Libasse Gueye wa Senegal akifunga manne akiwa na mchango mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba hadi sasa sambamba na Anicet Oura wa Ivory Coast aliyesajiliwa dirisha dogo la msimu huu.
Hii inaonyesha tofauti ya kimkakati ambapo Yanga wakitegemea mfumo wa timu nzima kushambulia, huku Simba wakitumia ufanisi na nidhamu ya kiufundi kupata matokeo ya ushindi.
Kwa miaka ya hivi karibuni, rekodi ya Kariakoo Derby imekuwa na ushindani mkali, lakini takwimu zinaipa Yanga nafasi ya kujiamini zaidi kutokana na mfululizo wa matokeo mazuri wanayopata wakikutana na wapinzani wao hao wa Kariakoo.
Hata hivyo, derby ina tabia ya kuvunja hesabu zote ndani ya dakika 90 ambapo historia inaweza kufutwa na kuandikwa upya kutokana na maandalizi na ufanisi wa kutumia nafasi kwa timu zote mbili.
Kinachofanya ratiba hii kuwa ya kipekee si tu ukubwa wa mechi, bali ukaribu wake kwani fainali ya Muungano inakuja siku chache kabla ya dabi ya Kariakoo ya Ligi Kuu ya NBC hali inayobadilisha kabisa maandalizi ya timu zote mbili.
Mshindi wa Zanzibar ataingia kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC akiwa na morali ya juu na ataweka presha kwa mpinzani kuelekea mchezo wa ligi huku anayeshindwa ataingia na hasira na atajaribu kulipiza kisasi hali inayofanya kuongeza joto la michezo hiyo hivyo basi mechi hizi mbili si matukio tofauti bali ni sura mbili za simulizi moja.
Kutoka visiwa vya Zanzibar hadi mitaa ya Kariakoo, Tanzania inajiandaa kushuhudia burudani ya kiwango cha juu, presha isiyo na mfano na historia mpya ikiandikwa kwa michezo miwili ya Kariakoo Derby kupigwa ndani ya wiki moja.
Swali linabaki kuwa moja tu:
Nani ataibuka kuwa mfalme wa wiki hii kati ya Simba au Yanga?