Ligi Kuu ya NBC imeendelea kutoa ushindani mkubwa huku timu mbalimbali zikipigania nafasi za juu na kujinusuru kwenye maeneo ya hatari na kumalizia msimu huu.
Mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar iliwakaribisha JKT katika dimba la Jamhuri mkoani Morogoro na mchezo huo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Mtibwa ilipata mabao yake kupitia Haroun Lwawatwa na Magata Fredrick huku JKT Tanzania ikiandika yake kupitia kwa Paul Peter aliyefunga yote mawili.
Mkoani Arusha uwanja wa Sheikh Amri Abeid TRA iliwakaribisha Fountain gate na kupoteza kwa mabao 2-1.
TRA ilikuwa ya kwanza kuandika bao kupitia kwa John Lazarus dakika ya 35 lakini dakika ya 44 Ismail Aziz aliwapatia bao la kusawazisha Fountain Gate na kuongeza lingine dakika moja kabla ya mapumziko lililohakikisha alama tatu muhimu kwa Fountain.
Kwa upande mwingine katika uwanja wa KMC jijini Dar es salaam Simba iliendelea kusalia kwenye mbio za ubingwa baada ya kuifunga Dodoma Jiji kwa bao 1-0 lililofungwa na Elie Mpanzu dakika ya 62.
Coastal Union ilikutana na Mashujaa kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga na kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 kupitia bao la Maabad Maabad dakika ya 65.
Matokeo haya yanaendelea kufanya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC kuwa wa ushindani zaidi huku Simba ikishikilia usukani kwenye msimamo na timu za katikati pamoja na za chini zikisaka alama muhimu kuelekea mwisho wa msimu.