MSHAMBULIAJI wa timu ya Kagera Sugar Obrey Chirwa hakamatiki hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kuwa kinara kwa kufunga mabao akiwa nayo 16 hadi sasa ndani ya Ligi ya Championship ya NBC.
Ligi hiyo imeshachezwa mizunguko 27 huku ikiwa imesalia mizunguko mitatu ili Ligi hiyo kufikia ukingoni ambapo pia mchezaji huyo ameisaidia timu yake kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwania kurejea Ligi Kuu ya NBC baada ya kukusanya alama 65.
Maulid Shaban wa Geita Gold hayupo mbali akiwa amefanikiwa kuifungia mabao 14 timu yake ambayo ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikikusanya alama 68.
Ramadhani Kalanje wa timu ya B19 nae ameweza kutikisa nyavu za wapinzani wao mara 13 huku timu hiyo ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo ikikusanya alama 31.
Abdereheman Mussa wa Transit Camp iliyopo nafasi ya tano kwenye msimamo na Emmanuel Mpuka wa Polisi Tanzania iliyopo nafasi ya tatu wameweza kufunga mabao 12 kila mmoja.
Adam Uledi aliyekuwa Transit Camp kabla ya kuhamia KMC ya Ligi Kuu ya NBC, Boniface Brown wa Mbeya Kwanza na Samson Kassian wa KenGold wamefanikiwa kufunga mabao 11 kila mmoja hadi sasa kwenye ligi hiyo.