‘WALINDA LANGO’ LA AZAM NI MOTO WA KUOTEA MBALI LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 imeendelea kushuhudia ushindani mkubwa si tu katika ufungaji wa mabao, bali pia katika uimara wa safu za ulinzi huku takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Azam ndiyo timu iliyocheza michezo mingi zaidi bila kuruhusu bao, ikifanikiwa kutofungwa katika michezo 20 hadi sasa.

Azam imeonyesha nidhamu kubwa langoni chini ya magolikipa wao Aishi Manula aliyecheza michezo 11 bila kuruhusu bao, Zuberi Foba aliyecheza michezo nane bila kuruhusu na Issa Fofana aliyefanya hivyo kwenye mchezo mmoja.

Mabingwa watetezi Young Africans wanafuatia kwa kutofungwa bao katika michezo 19 wakionyesha uimara mkubwa wa walinda mlango wao chini ya Djigui Diarra, Hussein Masalanga na Abutwalib Mshery.

Simba wanashika nafasi ya tatu kwa michezo 17 ya kutofungwa bao, huku Mashujaa wakishika nafasi ya nne kwa michezo 12, Dodoma Jiji wakikusanya michezo 11 ya kutofungwa bao na kujikita miongoni mwa timu zenye safu bora za golikipa msimu huu.

JKT Tanzania, TRA na Pamba Jiji zote zimefanikiwa kutofungwa bao katika michezo 10 kila moja, zikithibitisha uimara wao wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya wapinzani.

Orodha hii inaonyesha wazi kuwa mafanikio ya timu nyingi msimu huu hayajatokana na ushambuliaji pekee, bali pia uimara wa walinda mlango na mabeki ambao wamekuwa nguzo muhimu katika kupambania matokeo chanya ndani ya Ligi Kuu ya NBC.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *