Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo, kwa michezo mitatu muhimu ambayo inaweza kuathiri mbio za ubingwa, nafasi za juu kwenye msimamo pamoja na vita ya kujiokoa dhidi ya kushuka daraja.
Mbeya City na Mtibwa Sugar watacheza Saa 8:00 mchana Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku ‘wababe’ hao wa ‘Green city’ wakisaka alama muhimu ili kujiimarisha kwenye vita ya kuendelea kusalia Ligi Kuu.
Mashujaa na Young Africans watakutana Saa 10:15 alasiri kwenye dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Vinara wa ligi Young Africans watalenga kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo huku Mashujaa nao wakihitaji matokeo mazuri mbele ya mashabiki wao ili kuboresha nafasi yao kwenye jedwali.
JKT Tanzania na Singida Black Stars watakutana Saa 12:30 jioni kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo mkoani Dar es Salaam.
Huu unatarajiwa kuwa mchezo wa ushindani mkubwa kati ya timu mbili zinazowania nafasi za juu.
JKT Tanzania wanaingia wakiwa nafasi ya sita, huku Singida Black Stars wakishika nafasi ya nne, hivyo ushindi utakuwa muhimu kwa kila upande katika mbio za kumaliza msimu ndani ya nafasi za juu.
Mashujaa, Mbeya City na Mtibwa Sugar wanapatikana katika nusu ya chini ya msimamo na wanaendelea kupambana kujinusuru dhidi ya kushuka daraja.
Michezo ya leo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku kila timu ikiwa na malengo tofauti na baadhi zikisaka ubingwa, nyingine nafasi za juu, na nyingine zikihitaji pointi muhimu ili kuendelea kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC.