Ligi Kuu ya NBC msimu 2025/26 inaendelea leo Juni 27, kwa michezo nane itakayochezwa kwa wakati mmoja kuanzia saa 10:00 jioni.
Timu mbalimbali zinashuka dimbani zikiwa na malengo tofauti, ikiwemo kusaka ubingwa, nafasi za juu, pamoja na kupambana kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.
Ratiba ya mechi za leo ni kama ifuatavyo:
Dodoma Jiji dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma huku Tanzania Prisons inayopambana kusalia Ligi Kuu ya NBC msimu ujao dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Young Africans dhidi ya TRA United watacheza uwanja KMC Complex, jijini Dar es Salaam na Mashujaa dhidi ya KMC watacheza kwenye uwanja Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Pamba Jiji itaialika JKT Tanzania kwenye ‘dimba’ la CCM Kirumba jijini, Mwanza huku ‘mnyama’ Simba akiikaribisha Singida Black Stars kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam katika mchezo mkubwa wa siku ya leo.
Coastal Union dhidi ya Azam watacheza kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga na Namungo atakuwa na kibarua dhidi ya Fountain Gate mkoani Lindi katika uwanja wa Majaliwa.
Macho ya mashabiki wengi yataelekezwa kwenye mechi za Yanga dhidi ya TRA United na Simba dhidi ya Singida Black Stars, huku kila timu ikihitaji matokeo mazuri katika hatua za mwisho za msimu.
Ni siku muhimu kwa kila timu, ambapo kila alama inaweza kuwa na mchango mkubwa katika mbio za ubingwa, nafasi za juu, au vita ya kubaki Ligi Kuu ya NBC.