Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo imefanya semina ya kuwajengea uwezo maafisa habari wa klabu za Ligi Kuu ya NBC na Championship katika Ukumbi wa NSSF Mafao House, Ilala jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano nchini.
Akifungua semina hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Cornel Barnabas, aliwashukuru maafisa habari kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya soka nchini, akisisitiza kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya klabu, mashabiki na wadau mbalimbali wa mchezo huo.
Barnabas alisema maafisa habari wana jukumu la kuhakikisha taarifa za Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Championship ya NBC zinawafikia wadau kwa usahihi na kwa wakati, hatua inayochangia kujenga uelewa wa pamoja, kuimarisha taswira ya ligi na kukuza mchezo wa mpira wa miguu nchini.
“Semina hii ni fursa ya kujengana kitaaluma, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano ili tuendelee kuzifanya ligi zetu kuwa bora zaidi. Ni muhimu kuzingatia misingi na maadili ya uandishi wa habari pamoja na kuhakikisha taarifa zinazotolewa ni sahihi na zenye kuwajengea imani wadau wetu,”
Katika semina hiyo, Afisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, aliwasilisha mada kuhusu nafasi na majukumu ya vyombo vya habari akieleza umuhimu wa mawasiliano ya kitaalamu katika kukuza soka na kujenga uhusiano mzuri kati ya klabu, wadau na mashabiki.
Naye Meneja wa Chapa, Matukio na Udhamini wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Janeth Mbelwa aliwasilisha mada kuhusu usimamizi wa chapa, matukio na udhamini katika michezo.
Aliwataka maafisa habari kutambua nafasi yao katika kuongeza thamani ya ligi na wadhamini kupitia utoaji wa taarifa sahihi, maudhui yenye ubora na ushirikiano unaoimarisha taswira ya mashindano na washirika wa kibiashara.
Afisa habari wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Prudence Constantine, aliwasilisha mada kuhusu maadili ya taaluma ya uandishi wa habari, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia weledi, uwajibikaji na viwango vya taaluma katika utoaji wa habari.
Aidha, wataalamu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) waliwasilisha mada kuhusu mapambano dhidi ya rushwa katika michezo, wakieleza athari za vitendo vya rushwa kwa maendeleo ya soka na umuhimu wa kila mdau kushiriki katika kulinda misingi ya haki, uwazi na uadilifu katika mashindano.
Semina hiyo ililenga kuwajengea uwezo maafisa habari, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kuelekea msimu mpya wa mashindano, huku TPLB ikiendelea kusisitiza utoaji wa taarifa sahihi, zenye weledi na zinazochangia maendeleo ya soka nchini.