LIGI Kuu ya NBC imeendelea kushika kasi ambapo timu ya Polisi Tanzania iliikaribisha timu ya Azam katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana.
Mchezo huo ulichezwa majira ya saa kumi jioni ambapo ulikuwa muhimu kwa timu zote ikiwa ni mchezo wa kwanza wa msimu wa 2026/2027 hivyo timu zote zilitaka ushindi ili kuanza vyema msimu.
Mchezo ulianza kwa kasi kubwa huku timu zote zikishambuliana na kujilinda kuhakikisha hawaruhusu mpinzani kuingia katika lango lao na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna aliyefanikiwa kuingia katika lango la mwenzake.
Timu zilirejea na kasi kubwa ya kutafuta ushindi na dakika ya 79 Abdul Suleman wa Azam aliitanguliza mbele timu yake kupitia mkwaju wa penati baada ya mchezaji wa Azam kufanyiwa madhambi ambapo mwamuzi Hance Mabena alijiridhisha kupitia mfumo mpya wa kusaidia waamuzi (Football Video Support (FVS) na kutoa maamuzi.
Anuary Jabir wa Polisi Tanzania aliwanyanyua maafande hao baada ya kufunga bao la kusawazisha kupitia mkwaju wa penati pia baada ya mchezaji wa Polisi Tanzania kuchezewa madhambi na mwamuzi kujiridhisha kupitia FVS hivyo mchezo ulitamatika kwa timu hizo kugawana alama 1-1.