SIMBA YAJIPATA KAGERA, JKT, TRA ZAIDI YA MCHEZO.

MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC umetamatika jana kwa michezo miwili iliyopigwa mkoani Kagera na Dar es Salaam.

Mchezo wa kwanza ulichezwa uwanja wa Kaitaba ambapo timu ya Kagera Sugar ilikuwa mwenyeji wa timu ya Simba mchezo uliochezwa majira ya saa kumi jioni.

Mchezo ulianza kwa kasi kubwa huku timu zote zikiwa na ari kubwa ya kutaka alama tatu muhimu ili kuanza vyema katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa Kagera Sugar imerejea baada ya kucheza Championship msimu uliopita na kushika nafasi ya pili.

Ilimchukua dakika 45 beki wa Simba Ismail Traore kufungua ukurasa wa mabao baada ya kuruka na kufanikiwa kufunga bao la kichwa na timu zilienda mapumziko 0-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi Kagera Sugar ikitaka kusawazisha huku Simba ikitaka kuongeza bao ambapo dakika ya 68 Elie Mpanzu aliongezea bao timu yake hivyo mchezo kutamatika kwa 0-2 na kiungo wa Simba Libase Gueye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Mchezo wa pili ulikuwa kati ya JKT Tanzania dhidi ya TRA United ulichezwa katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo majira ya saa mbili na nusu usiku.

Kipindi cha kwanza kilianza huku TRA wakitawala mchezo kwa dakika zote 45.

Dakika 13 pekee zilimtosha Tobias Omondi wa TRA kufungua ukurasa wa mabao ambapo mchezo huo ulienda mapumziko kwa 0-1.

Kipindi cha pili JKT Tanzania walionekana wakitawala mchezo ambapo dakika ya 50 walisawazisha kupitia mchezaji wao Godfrey Luzendaze na matokeo yalisalia 1-1 mpaka mchezo unatamatika huku mchezaji wa TRA Joseph Akandwanaho alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *