POLISI, YANGA, AZAM ZAVUNA ALAMA LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo mitatu iliyochezwa katika viwanja vya Arusha na Dar es Salaam, huku Polisi Tanzania, Young Africans na Azam zikivuna ushindi.

 

Mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha uliwakutanisha Polisi Tanzania na JKT Tanzania, ambapo Polisi Tanzania iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

 

Polisi Tanzania ilianza kupata bao katika dakika ya 45+2 kupitia Kenny Ally, kabla ya Habib Kyombo kuongeza bao la pili dakika ya 65 na kuipa timu yake ushindi wa nyumbani.

 

Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, Young Africans iliendelea na matokeo mazuri baada ya kuichapa Coastal Union mabao 4-1.

 

Albert Kangandwa aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 37, huku Maxi Nzengeli akiongeza la pili dakika ya 45+4.

 

Yanga iliendelea kutawala mchezo na kuongeza mabao mawili kupitia Mudathir Yahya dakika ya 49 na Mohamed Hussein dakika ya 90+5.

 

Coastal Union ilipata bao lake pekee dakika ya 77 kupitia Gradi Lassa.

 

Coastal Union ilimaliza mchezo ikiwa na wachezaji 10 baada ya Geoffrey Manyasi kuonyeshwa kadi nyekundu.

 

 

Katika mchezo wa usiku uliochezwa saa 3:00 katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya TRA United.

 

Azam ilianza kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya 8 kupitia Iddi Selemani, kabla ya Abdul Suleiman kuongeza bao la pili dakika ya 33.

 

TRA United ilipunguza pengo dakika ya 45 kupitia Ousmane Kamisoko na kufanya mchezo kuendelea kuwa na ushindani.

 

Azam ilimaliza mchezo ikiwa na changamoto baada ya mlinda mlango wake, Aishi Manula, kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kufanya rafu.

 

Pamoja na kucheza pungufu, Azam iliweza kulinda uongozi wake hadi dakika ya mwisho na kuondoka na alama tatu muhimu.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *