MBEYA CITY, SIMBA ZAGAWA ‘DOZI’, KAGERA YABANWA NYUMBANI.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo mitatu iliyochezwa mkoani Mbeya, Mwanza na mkoani Kagera.

Mchezo wa kwanza uliwakutanisha mbeya city na Dodoma jiji na ‘wababe’ wa Mbeya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye uwanja wa Sokoine.

Wenyeji hao walihitaji dakika 9 pekee kuandika bao la kwanza kupitia kwa Mwani Thobias, kabla ya Yahya Mbegu kuifungia Mbeya City bao la pili dakika ya 72 na kuifanya Dodoma Jiji kuondoka Mbeya mikono mitupu.

Mchezo mwingine uliovuta hisia ulipigwa saa 10:15 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ambapo Simba ilikuwa ugenini dhidi ya Pamba Jiji na kupata ushindi wa mabao 2-1.

Simba ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 19 kupitia Clatous Chama, kabla ya Anicet Oura kuongeza bao la pili dakika ya 31.

Hata hivyo, mambo yalibadilika kwa Simba dakika ya 39 baada ya Ibraheem Jabaar kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kucheza vibaya na hivyo Simba kulazimika kuendelea na mchezo ikiwa na wachezaji pungufu.

Pamba Jiji ilitumia nafasi hiyo kuongeza presha na hatimaye kupata bao la kufutia machozi dakika ya 72 kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Diomande Idris.

Licha ya Pamba Jiji kusukuma mashambulizi katika kipindi cha mwisho, Simba iliweza kusimama imara na kulinda ushindi wake hadi filimbi ya mwisho

Mkoani Kagera, katika Uwanja wa Kaitaba, mchezo mwingine wa kusisimua uliwakutanisha Kagera Sugar na Singida Black Stars uliomalizika kwa sare ya 1-1.

Kagera Sugar ilianza vyema na kupata bao dakika ya 13 kupitia Kassim Feka, hali iliyowapa wenyeji matumaini ya kuondoka na alama zote.

Hata hivyo, Singida Black Stars haikukubali kushindwa na ilirejea kipindi cha pili kwa nguvu zaidi.

Juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 50 baada ya Jonathan Sowa kuisawazishia timu yake.

Bao hilo liliifanya mechi kuwa ya ushindani zaidi, huku pande zote zikisaka bao la ushindi, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda hadi dakika za mwisho.

Kwa ujumla, michezo hiyo imeendelea kuonyesha ushindani mkubwa , huku Mbeya City ikifurahia ushindi wa nyumbani, Simba ikivuna alama ugenini licha ya kucheza pungufu, na Kagera Sugar pamoja na Singida Black Stars zikigawana alama katika Uwanja wa Kaitaba.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *