Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Agosti 21, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
Ligi Kuu ya NBC
Mechi Namba 001: Pamba Jiji 1-1 Dodoma Jiji
Klabu ya Dodoma Jiji imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wachezaji wake kuonekana wakifanya kitendo kinachoashiria imani za kishirikina kuelekea mchezo tajwa hapo juu.Wakati wa kufanya mazoezi Wachezaji hao walijikusanya Katikati ya uwanja na kuweka duara kuashiria kuomba dua lakini mmoja kati ya wachezaji hao alionekana akichimbia vitu chini.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 48:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Klabu ya Pamba Jiji imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuelekea mchezo tajwa hapo juu Agosti 14, 2026.Pamba iliwasili uwanjani saa 6:51 Mchana badala ya saa 6:30 Mchana jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 0010: Namungo 1-0 Geita Gold
Klabu ya Namungo imepewa onyo kali kwa kosa la vijana waokota mipira (Ball Boys) kuficha mipira na wakati mwingine kutoifata kabisa pindi mipira hiyo ilivyotoka nje. Kitendo hicho si cha kiungwana na kiuanamichezo, Kamati inatoa angalizo kwa klabu zote kuheshimu na kuzingatia kanuni ya Uchezaji wa Kiungwana.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 0012: Pamba Jiji 1-2 Simba SC
Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu wakati wa mapumziko hali iliyofanya waamuzi hao kushindwa kutumia vyumba vya kubadilishia nguo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 48:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mchezaji wa Simba Ibraheem Jabaar ametozwa faini ya Sh 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji jezi namba 35 (Abdulkarim Iddy) pamoja na hiyo, adhabu ya kadi nyekundu itaendelea kubaki kama ilivyo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:5(5.2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mechi Namba 0013: Kagera Sugar 1-1 Singida BS
Mchezaji wa Singida BS Mathew Tegisi amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Kagera Sugar jezi namba 12 (Salehe Seif).
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:5(5.2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Tatu Malogo kutoka Tanga amepewa Onyo Kali kwa kosa la kuonesha mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
TAARIFA MAALUM
Kamati inazikumbusha timu zote kuzingatia kikamilifu masharti ya Kanuni ya 20 kuhusu Matumizi ya Teknolojia ya Football Video Support System (FVS).Kwa mujibu wa Kanuni ya 20(4), ni Kocha Mkuu au kiongozi mwingine wa juu kwenye benchi la ufundi pekee mwenye haki ya kuwasilisha ombi la marejeo ya tukio katika FVS, kwa kuwasiliana na Mwamuzi wa Akiba (Fourth Official).
Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 20(4)4.1, iwapo mchezaji ataona tukio linahitaji marejeo ya FVS, anatakiwa kuwasiliana kwa ishara na Kocha Mkuu au kiongozi wa benchi la ufundi, ambaye ndiye atakayewasilisha ombi hilo.
Ni marufuku kwa mchezaji kumkabili, kumlalamikia au kumshinikiza mwamuzi moja kwamoja kwa lengo la kuomba marejeo ya FVS. Mchezaji atakayekiuka masharti hayo ataadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62.
Kamati itaendelea kusimamia utekelezaji wa kanuni hizi, na adhabu zitatolewa dhidi ya watakaobainika kukiuka masharti yaliyowekwa.