GEITA ‘YAUA’ BUKOMBE, SIMBA IKIENDELEZA UBABE LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo miwili iliyotoa burudani kubwa kwa mashabiki, Singida Black Stars waliwakaribisha simba na kupoteza 1-2 kwenye uwanja wa Airtel mkoani Singida huku Geita Gold ikianza vyema kwenye uwanja wake mpya kwa ushindi mnono wa mabao 6-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Clatous Chama aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 12, Sheikhah Ibrahim wa singida akaweka mzani sawa dakika ya 22 na kuwainua mashabiki wa Singida.

Hata hivyo, Simba ilirejea ikiwa na nguvu zaidi kipindi cha pili na kufanikiwa kuongoza mchezo kupitia Rushine De Reuck, aliyefunga dakika ya 62.

Mchezo huo pia ulishuhudia Simba ikicheza ikiwa pungufu baada ya Anthony Mligo kuonyeshwa kadi nyekundu na kuwa mchezo wa tatu mfululizo Simba kupata kadi nyekundu tangu ligi ianze.

Katika mchezo mwingine uliochezwa Uwanja wa kisasa wa Bukombe, mkoani Geita, ambapo Geita Gold ilianza kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Mchezo huo ulikuwa wa kipekee kwa timu hizo mbili ambazo zimepanda kutoka Championship na kushiriki Ligi Kuu, huku ikiwa pia ni mara ya kwanza kwao kucheza katika uwanja huo mpya uliopo Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, ambao Geita Gold inautumia kama uwanja wake wa nyumbani.

Geita Gold ilianza kuandika historia hiyo dakika ya 10 kupitia Richard N’gondya, kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 23 kupitia Obrey Chirwa kwa mkwaju wa penalti.

Yussufu Mhilu aliendelea kuipa Geita Gold nguvu kwa kufunga dakika ya 34 na 46, huku Richard N’gondya akifunga bao lake la pili katika mchezo huo dakika ya 63.

Chirwa alikamilisha siku yake nzuri kwa kufunga bao la pili dakika ya 69 na kuifanya Geita Gold kufikisha mabao sita.

Kagera Sugar ilipata mabao mawili ya kufutia machozi, yakifungwa na Hassan Mwatelema dakika ya 40 na Robert Mkandya dakika ya 90+1.

Ushindi huo unaifanya Geita Gold kuanza safari yake ya Ligi Kuu kwa kiwango cha kuvutia, huku mchezo huo ukitoa burudani kubwa kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia historia ya timu hizo kwenye uwanja mpya.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *