LIGI Kuu ya NBC imezidi kupamba moto ikiwa ni mzunguko wa sita kwa timu ya Simba huku kwa Azam wakicheza mzunguko wa saba, ambapo timu ya Azam ilikuwa mwenyeji wa timu ya Simba kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar.
Hadi mapumziko timu hizo zilienda bila upande wowote kupata bao ingawa Simba walionyesha uhai kwenye nafasi ya ushambuliaji kwa kutengeneza nafasi nyingi kuliko wenyeji.
Kipindi cha pili Simba ilianza kwa kasi na dakika ya 58 ilifungua akaunti ya mabao baada ya Nathan Idumba kujifunga na kuifanya Simba kuongoza 1-0.
Wekundu wa Msimbazi waliendelea kutawala mchezo na kuongeza bao la pili dakika ya 68 likifungwa na Clatous Chama.
Licha ya Azam kutafuta njia ya kurejea mchezoni, safu ya ulinzi ya Simba ilifanikiwa kulinda lango lake hadi dakika 90 na kuifanya Simba kumaliza mchezo kwa ushindi wa mabao 2-0 na kukusanya alama tatu.
Baada ya michezo huo Ligi Kuu ya NBC itasimama kwa wiki mbili inatarajiwa kurejea oktoba 8, 2026.