TAARIFA YA KAMATI YA UENDESHAJI NA USIMAMIZI WA LIGI YA BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB).

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Oktoba 6, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi ya Championship ya NBC

 Mechi Namba 009: Mbeya Kwanza 1-2 Tanzania Prisons

 Klabu ya Mbeya Kwanza imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (Milioni Tano) kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye uwanja wa mchezo tajwa hapo juu. Mbeya Kwanza iliwasili saa 8:47 mchana badala ya saa 8:30 mchana kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:61 Kuhusu Taratibu za mchezo.

 Mechi Namba 015: Songea United 0-0 Rhino Rangers

Klabu ya Songea United imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (Milioni Tano) kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye uwanja wa mchezo tajwa hapo juu. Songea United iliwasili saa 8:58 mchana badala ya saa 8:30 mchana kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:61 Kuhusu Taratibu za mchezo.

 Mechi Namba 021: Mbeya Kwanza 2-1 Bandari Tanzania

Klabu ya Mbeya Kwanza imepewa Onyo Kali kwa kosa kushindwa kuandaa mchezo kikamilifu ambapo Gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) lilichelewa kuwasili uwanjani hali iliyopelekea mchezo huo kuchelewa kuanza kwa dakika 15 kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:7 kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:61 Kuhusu Taratibu za mchezo.

Mechi Namba 023: Tanzania Prisons 2-0 Mbuni FC 

Mtunza Vifaa wa Klabu ya Mbuni Christopher Joseph ametozwa Faini ya Sh. 1,000,000 (Milioni Moja) kwa kosa la kumwaga vimiminika kwenye maeneo mbalimbali ya uwanja wakati timu hizo zikiwa zinapasha misuli joto (Warm Up) kitendo kilichotafsiriwa kama Imani za kishirikina.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 45:2(2.4) kuhusu Udhibiti kwa Makocha na Maofisa wengine wa Ufundi.

Wachezaji, Michael Mpesa wa Tanzania Prisons na Ezekiel Eusebio wa Mbuni wametozwa Faini ya Sh. 1,000,000 (Milioni Moja) kila Mmoja kwa kosa la kukataa kutoka uwanjani wakati wa mapumziko wa mchezo tajwa hapo juu kitendo kilichotafsiriwa kama Imani za kishirikina. Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 41:5 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mechi Namba 026: Transit Camp 3-1 IAA SC

Klabu ya Transit Camp imetozwa Faini ya Sh. 5,000,000 (Milioni Tano) kwa kosa la Vijana waokota mipira (Ball Boys) wa timu hiyo kwa makusudi kuchelewesha kurudisha mipira uwanjani pale ilipokuwa inatoka nje ya uwanja licha ya kuonywa mara kadhaa na mwamuzi wa mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:61 Kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 026: Tanzania Prisons 1-0 Songea United   

Klabu ya Songea United imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) kuelekea mchezo tajwa hapo juu kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:2 Kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:61 Kuhusu Taratibu za Mchezo.

Wachezaji wa Songea United, Ramadhani Kapera, Gilbert Boniface Pamoja na Daktari wa timu hiyo Shabani Mbotohii wametozwa faini ya Sh. 1,000,000 kila mmoja kwa kosa kumwaga vimiminika kwenye maeneo mbalimbali ya uwanja kitendo kilichotafsiriwa kama Imani za Kishirikina. Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 41:5 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji na 45:2(2.4) kuhusu Udhibiti kwa Makocha na Maofisa wengine wa Ufundi.

Mechi Namba 029: Mtibwa Sugar 1-0 Mbeya Kwanza

Klabu ya Mtibwa Sugar imetozwa Faini ya Sh. 1,000,000 (Milioni Moja) kwa kosa la mashabiki wake kumrushia mawe mwamuzi msaidizi namba mbili wa mchezo huo Hudson Samwel. Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 Kuhusu Udhibiti kwa Klabu

Mechi Namba 032: Bandari Tanzania 1-1 KMC FC

Klabu ya Bandari Tanzania imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (Milioni Tano) kwa kosa la mashabiki wake kuingia kwenye eneo la kuchezea baada ya mchezo kumalizika kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:18 kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:61 Kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mwamuzi wa kati Ikram Nguyahambi kutoka Tabora na Mwamuzi Msaidizi namba moja Haruna Shammea kutoka Tanga Wamefutwa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2026/2027 kwa kosa la kuonesha mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu kwenye mchezo tajwa hapo juu. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

 

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *