SIMBA YAZIDI KUJIKITA KILELENI LIGI KUU YA NBC.

SIMBA imeendelea kuwa kinara kwenye Ligi Kuu ya NBC mzunguko wa nane baada ya kuichapa Mashujaa mabao 6-1 katika mchezo uliopigwa Oktoba 13, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifanya Simba kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na alama 24 baada ya kushinda michezo yote nane iliyocheza hadi sasa huku ikiendelea kuonyesha nia ya dhati katika mbio za kuwania ubingwa wa msimu huu.

Simba ilianza mchezo kwa kuonyesha dhamira ya kutafuta ushindi, ikimiliki mpira na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kuelekea langoni mwa timu ya Mashujaa.

Dakika ya 16, Libasse Gueye alifungua ukurasa wa mabao kwa shuti kali la mguu wa kushoto kutoka nje ya eneo la hatari, akimalizia pasi saidizi ya Neo Maema.

Dakika ya 33, Elie Mpanzu aliandika bao la pili kwa timu hiyo baada ya kumalizia krosi iliyopigwa na Nathaniel Chilambo, na kuifanya Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Hali ya Mashujaa ilizidi kuwa ngumu baada ya Hassan Kabunda kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza, jambo lililoifanya timu hiyo kuendelea na mchezo ikiwa na wachezaji pungufu.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuongeza kasi ya mashambulizi na kuutumia vizuri mwanya uliokuwepo dhidi Mashujaa.

Anicet Oura alifunga bao la tatu dakika ya 54, kabla ya Mpanzu kuongeza bao lake la pili katika mchezo huo dakika ya 58 na kuifanya Simba kuongoza kwa mabao 4-0.

Morice Abraham alifunga bao la tano dakika ya 60, akiendeleza shinikizo la Simba dhidi ya wapinzani wao.

Hata hivyo, Mashujaa hawakukubali kuondoka bila kupata bao ambapo mshambuliaji wao Seleman Bwenzi aliifungia timu yake bao la kufutia machozi dakika ya 63 kwa shuti kali kutoka nje ya eneo la hatari, na kufanya matokeo kuwa 5-1.

Simba haikuridhika na matokeo hayo dakika ya 69, Ismail Toure alifunga bao la sita kwa shuti la chini la mguu wa kushoto baada ya kupokea pasi ya Ibraheem Jabaar na kuhitimisha ushindi mnono wa mabao 6-1.

Kiungo wa Simba Ellie Mpanzu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango kizuri.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *