Michezo miwili ya raundi ya 11 ya Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27 imeshuhudia Coastal Union na Dodoma Jiji zikigawana alama baada ya kutoka suluhu na Azam kupata ushindi ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya ‘maafande’ wa JKT.
Katika mchezo uliichezwa kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani mkoani Tanga saa 10:00 alasiri, Coastal Union na Dodoma Jiji zimeshindwa kupata bao dakika zote 90 na matokeo yalifanya kila timu kuondoka na alama moja.
Katika mchezo huo, mchezaji wa Dodoma Jiji , Iddy Kipagwile, alifunga bao ambalo lilikataliwa na mwamuzi wa mchezo huo kutokana na faulo iliyotokea kabla ya mpira kutinga nyavuni.
Yesse Kibamba wa Dodoma Jiji alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonesha kiwango bora.
Katika mchezo mwingine uliochezwa kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, JKT waliwakaribisha Azam kwenye uwanja wao wa nyumbani mchezo ulichezwa saa 12:30 jioni.
JKT Tanzania ndiyo ilianza kupata bao kupitia kwa Karim Mfaume dakika ya 13 kabla ya Iddi Seleman kuisawazishia Azam dakika ya 29.
Lusajo Mwaikenda aliihakikishia Azam ushindi baada ya kufunga bao la pili dakika ya 59 kwa ‘utosi’ bao lililompa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuamua matokeo.
Ushindi huo unaipa Azam alama zote tatu, na huku Coastal Union na Dodoma Jiji zikigawana alama moja kila moja katika mchezo wa raundi ya 11.