LIGI KUU YA NBC MWENDO MDUNDO

Ligi Kuu ya NBC raundi ya pili imetamatika jana Agosti 21, 2022 kwa michezo minne kuchezwa na kukamilisha jumla ya michezo minane katika raundi ya pili.

Mchezo wa mapema ulizikutanisha Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting saa 8:00 mchana katika uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro na Mtibwa Sugar kushinda kwa mabao 2-1. Michezo miwili ya saa 10:00 ilizikutanisha Polisi Tanzania na KMC FC kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha ukimalizika kwa sare ya mabao 2-2 huku ule wa Singida Big Stars na Mbeya City ukimalizika kwa Singida kuibuka na Ushindi wa mabao 2-1.

Mchezo wa Azam FC dhidi ya Geita Gold uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex majira ya saa 1:00 usiku ndio ulikuwa mchezo wa mwisho kwa raundi ya pili na kumalizika kwa sare ya bao moja.

Simba SC inaendelea kubaki kileleni ikiwa na alama sita ikifuatiwa na Yanga SC yenye alama sita, nafasi ya tatu inashikiliwa na Singida BS ikiwa na alama sita huku utofauti ukiwa katika mabao ya kufunga na kufungwa.

Mabao 20 yamefungwa  katika raundi ya pili na kufanya jumla ya mabao 40 yawe yamefungwa hadi sasa ndani ya msimu huu wa 2022/2023, Reliants Lusajo ndiye anayeongoza mbio za ufungaji akiwa amefunga mabao matatu akifuatiwa na Salum kipemba, Fiston Mayele, Matheo Anthony, Moses Phiri, Nassor Kiziwa, Sixtus Sabilo na Tepsie Evance wakiwa na mabao mawili kila mmoja.

Mpaka hivi sasa ni Ihefu SC pekee ndio ambao hawajafunga bao lolote huku Simba SC ikiwa ndio timu pekee ambayo haijaruhusu bao.

Ligi Kuu ya NBC imesimama hadi Septemba 6, 2022 kupisha mechi za timu ya taifa kuwania kufuzu michuano ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *